(+Picha) Rais Kenyatta azindua hospitali 5 jijini Nairobi katika ziara ya masaa 4 usiku

Rais alisema kuwa aliamua kuzindua hospitali hizo usiku ili kuzingatia itifaki za kuzuia maambukiza ya COVID 19.

Muhtasari

•Vituo vya afya ambavyo rais alizindua katika ziara yake ni zahanati ya Gichagi iliyo Kangemi na Gatina iliyo Kawangware pamoja  na hospitali za Mukuru kwa Rueben, Tassia Kwa Ndege na Our Lady of Nazareth iliyo Mukuru Kwa Njenga.

•Tano hizo ni kati ya hospitali 24 ambazo zinajengwa jijini  na huduma ya mji mkuu wa Nairobi(NMS) kama njia ya kupunguza idadi ya wagonjwa katika hospitali kuu ya Kenyatta, Mama Lucy, Pumwani na Mbagathi.

Rais Kenyatta azindua zahanati ya Gatina iliyo Kawangware usiku wa Jumanne
Rais Kenyatta azindua zahanati ya Gatina iliyo Kawangware usiku wa Jumanne
Image: HISANI

Rais Uhuru Kenyatta alizindua hospitali tano mpya jijini  Nairobi katika ziara ya ya masaa manne usiku wa Jumanne na kuelekeza ziwape wakazi huduma ya masaa 24.

Tano hizo ni kati ya hospitali 24 ambazo zinajengwa jijini  na huduma ya mji mkuu wa Nairobi(NMS) kama njia ya kupunguza idadi ya wagonjwa katika hospitali kuu ya Kenyatta, Mama Lucy, Pumwani na Mbagathi.

Vituo vya afya ambavyo rais alizindua katika ziara yake ni zahanati ya Gichagi iliyo Kangemi na Gatina iliyo Kawangware pamoja  na hospitali za Mukuru kwa Rueben, Tassia Kwa Ndege na Our Lady of Nazareth iliyo Mukuru Kwa Njenga.

Rais aliyekuwa ameandamana na mkurugenzi mkuu wa NMS, Mohammed Badi alielekeza hospitali hizo kuhudumia wakazi wakati wowote wanapohitaji matibabu.

"Zahanati na hospitali zinafaa kutoa huduma ya masaa 24 ili kupunguza wagonjwa katika hospitali ya Kenyatta na ya Mama Lucy. Badala ya mtu kutumia pesa kuenda kutafuta huduma za afya KNH wanafaa kuweza kupata huduma hizo katika hospitali zilizo karibu nao" Rais alisema.

Rais alisema kuwa aliamua kuzindua hospitali hizo usiku ili kuzingatia itifaki za kuzuia maambukiza ya COVID 19.

Alitangaza kuwa hospitali 19 kati ya 24 ambazo zinajengwa zimekamilika tayari na kusema kuwa mipango ya kuziandaa kuhudumia wananchi imeng'oa nanga.

Kando na kuzindua hospitali, rais alisema kuwa katika ziara yake alilenga pia kukagua ujenzi wa barabara ambao unaendelea mitaani na kusema kuwa tayari kilomita 400 zimekamilika huku ujenzi wa zingine  450 ukiendelea.

Aitangaza kuwa serikali inapanga kujenga kilomita zingine 300 za barabara mitaani mwaka huu wa fedha.

Rais alisema kuwa serikali imejitolea katika kuwapa wananchi huduma bora bila kuangazia hadhi yao maishani. 

Alisema kuwa NMS imechimbua mamia ya mabwawa ya maji jijini ambayo yanawapa wakazi maji safi.

"Leo hii mitaani hakuna suala ya watu kulipia maji. Watu walikuwa wanalipia shilingi 20 kupata mtungi wa maji lakini sasa tumewachimbulia mabwawa" Rais alisema.

Alisema kuwa upanuzi wa mifumo ya maji taka ambao unaendelea utafaidi mitaa duni ya Nairobi.