SIASA ZA 2022

Sitaki kupendekezwa na rais Uhuru ama mtu yeyote- Raila

Raila alisema kuwa iwapo ataamua kugombea urais hatatafuta pendekezo la rais ila atakachotaka ni kura yake tu.

Muhtasari

•Akiwa kwenye mahojiano katika stesheni moja ya redio nchini,  Raila amesema kuwa hajawahi kutegemea yeyote kumpendekeza anapowania kiti chochote.

•Raila pia alieleza imani yake kuwa BBI itarejea huku akisema kuwa bado kuna nafasi ya kura ya maoni kufanyika ili kurekebisha katiba kabla ya uchaguzi mkuu.

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: Hisani

Kinara wa ODM Raila Odinga amepuuzilia mbali madai kuwa anataka rais Uhuru Kenyatta ampendekeze kama mridhi mwafaka wa kiti atakachokipungia buriani mwaka ujao.

Akiwa kwenye mahojiano katika stesheni moja ya redio nchini,  Raila amesema kuwa hajawahi kutegemea yeyote kumpendekeza anapowania kiti chochote.

"Sijasema na hata Uhuru mwenyewe hajasema atapendekeza mtu. Mimi sitaki kupendekezwa na Uhuru ama mtu yeyote.Uhuru si unajua tulishindana na yeye, atanipendekeza namna gani?" Raila alisema.

Raila alisema kuwa ushirikiano wake na rais ni wa kikazi tu ila sio wa kisiasa. Alisema kuwa alikubali kumsaidia Uhuru kutekeleza ahadi zake kwa Wakenya.

"Yeye tumekuwa naye na tukaongea mambo mengi kirefu. Alinieleza shida ambazo alipata kipindi kile cha kwanza . Akasema kuwa sasa anataka kuleta mabadiliko ili aweze kutimiza ile ahadi ambayo alipatia Wakenya kisha aende nyumbani na nikasema ni sawa mimi naheshimu hayo" Raila aliendelea kusema.

Ingawa alisita kuzungumzia mipango yake ya kisiasa akisema kuwa atazungumza baada ya kura  ya maoni, Raila alisema kuwa iwapo ataamua kugombea urais hatatafuta pendekezo la rais ila atakachotaka ni kura yake tu.

"Sitaki kupendekezwa na Uhuru. Ile mimi nitataka ni kura  yake" Raila alisema.

Raila pia alieleza imani yake kuwa BBI itarejea huku akisema kuwa bado kuna nafasi ya kura ya maoni kufanyika ili kurekebisha katiba kabla ya uchaguzi mkuu.