'Dalili ya mvua ni mawingu,'Seneta Sakaja asema huku akimpigia Mudavadi debe

Siasa za Urithi wa Urais baada ya kipindi cha Rais Uhuru Kenyatta kukamilika Agosti mwaka ujao zinazidi kunoga huku kinara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi kwa siku ya pili akikita kambi maeneo ya Eastlands jijini Nairobi.

Baada ya kukutana na waumini wa kanisa la SDA Mathare North, eneo bunge la Embakasi siku ya JUmamosi na kisha kuhutubia wananchi wa Mathare North, Mudavadi hii leo  amejumuika na waumini wa kanisa la Jesus Teaching Ministry, Embakasi West kwa Ibaada ya Jumapili.

Huku akiwa na wabunge wa chama cha ANC, wabunge hao walidai kwamba hamna haja ya kufufua muungano wa NASA.

Huku seneta wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja akimpigia Mudavadi debe alimshauri kigogo huyo kwamba wakenya wanahitaji amani na matumaini.

Pia alisema kwamba dalili ya mvua ni mawingu na mwenye macho haambiwi tazama, kwa sababu Mudavadi ni wa NASA naye ni wa chama cha JUbilee.

Pia aliweka wazi kwamba anajivunia kuwa mwanachama wa Jubilee.

“Mkiona natembea na Musalia Mudavadi basi mwenye macho atazame, mwenye maskio asikie kwani dalili za mvua ni mawingu.

Tunatembea tukihubiri amani. Mheshimiwa Musalia najua wewe uko NASA mimi niko Jubilee na najivunia kuwa katika chama cha Jubilee.

Lakini kuna kitu nataka kukuambia katika JUbilee na kila mahali watu wanapokuona wanaona matumaini na maisha yao ya kesho

Wakenya wanataka Amani na Pesa. Tarajia kujenga ushirikiano mpya hebu tuwe marafiki wapya. Kwa maono ambayo tunayo tunapaswa kutazama siku zijazo," Johnson Sakaja Aliongea.