Matayarisho ya 2022; Mtangazaji Jalang'o ajiunga rasmi na ODM

Miezi miwili iliyopita Jalang'o alitangaza hadharani azma yake kuwania kiti cha ubunge maeneo ya Lang'ata

Muhtasari

•Jalang'o alikabidhiwa cheti cha uanachama na katibu mkuu wa chama hicho, Edwin Sifuna siku ya Alhamisi.

•Kwa sasa kiti hicho kimekaliwa na Nixon Kiprotich Korir wa Jubilee na ambaye ni mwandani mkubwa wa naibu rais William Ruto.

Image: TWITTER//ODM

Mtangazaji na mcheshi mashuhuri nchini Felix Odhiambo Odiwour almaarufu kama Jalang'o amejiunga rais na chama cha ODM.

Jalang'o alikabidhiwa cheti cha uanachama na katibu mkuu wa chama hicho, Edwin Sifuna siku ya Alhamisi.

"Mcheshi na mtangazaji wa radio Felix Odhiambo Odiwour almaarufu kama Jalang'o leo hii amejiunga na chama kikubwa zaidi cha kisiasa nchini Kenya. Alikabidhiwa cheti cha uanachama na SG Edwin Sifuna. Tunaendelea kusonga mbele" ODM ilitangaza.

Haya yanajiri huku ikiwa  imesalia mwaka mmoja tu uchaguzi mkuu kufanyika nchini.

Miezi miwili iliyopita Jalang'o alitangaza hadharani azma yake kuwania kiti cha ubunge maeneo ya Lang'ata, Nairobi.

Chama hicho ni maarufu sana katika eneo bunge la Lang'ata kwani hata kinara wake, Raila Odinga alikuwa mbunge pale hapo awali. 

Kwa sasa kiti hicho kimekaliwa na Nixon Kiprotich Korir wa Jubilee na ambaye ni mwandani mkubwa wa naibu rais William Ruto.