Wakili Willie Kimani na wahasiriwa wengine 2 wangekuwa hai ikiwa Sylvia Wanjiku angeripoti kutekwa nyara kwao

Muhtasari

Wakili Willie Kimani na wahasiriwa wengine 2 bado wangekuwa hai ikiwa Sylvia Wanjiku angeripoti kutekwa nyara kwao

willie.kimani
willie.kimani

HABARI NA ANNETTE WAMBULWA;

Kimani aliuawa kikatili pamoja na mteja wake Josephat Mwenda na dereva Joseph Muiruri baada ya kutekwa nyara walipokuwa wakitoka katika Mahakama ya Sheria ya Mavoko mnamo Juni 23, 2016.

Maafisa wanne wa AP Fredrick Leliman, Stephen Cheburet, Sylvia Wanjiku na Leonard Mwangi na mpasha habari wa polisi Peter Ngugi walikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya watatu hao.

Ofisa wa uchunguzi Nicholas Olesena ameambia korti asubuhi ya leo kwamba Wanjiku alipaswa kuripoti wakati watatu hao walinunuliwa ndani ya seli.

Olesena alikuwa akihojiwa na wakili Katwa Kigen ambaye anataka kumtoa Wanjiku katika kesi ya mauaji.

Katwa alitaka kujua ni kwanini Olesena aliamua kumshtaki wakati hakuna sababu inayomuunganisha na mauaji hayo.

Olesena alimwambia Jaji Jessie Lessit kwamba walimshtaki kwa sababu alikuwa sehemu ya njama hiyo na alikuwa msaidizi wa mauaji ya hao watatu.

"Sylvia alikuwa kazini siku hiyo, ikiwa angeweza kuripoti kwamba wahasiriwa walikuwa kwenye seli hatungekuwa hapa leo" alisema.

Alisisitiza kuwa ingawa hawakupata chochote kinachomuunganisha na watu waliokufa alicheza jukumu kwa kutoripoti juu yao kushikiliwa kwenye seli bila kuandikishwa.

"Alikuwa kazini wakati wahanga walipopelekwa huko, alijua wapo," Olesena alisema.

Korti pia ilisikia kwamba Wanjiku ndiye mtu aliyekuwa na funguo za seli.

Walakini, Olesena alisema katika Uchunguzi wao hawakupata kitu kingine chochote kinachomuunganisha na mauaji hayo.

Alipoulizwa ikiwa aliwekwa katika eneo la mauaji, alisema hawakupata ushahidi wowote unaomweka katika eneo la mauaji katika eneo la Soweto.

Pia alithibitishia korti kwamba wakati wa kuchunguza kitabu cha simu cha Peter Ngugi na Facebook hawakupata mawasiliano yoyote kati yao.

Ngugi ndiye mpelelezi wa polisi ambaye alikiri na kusababisha kukamatwa kwa maafisa wengine.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Alhamisi wiki ijayo.