Barasa akana kumzaba kofi mwanakandarasi, adai aliona uchi wake akaenda kumwambia afunge zipu

Masinde ambaye pia ni mwanamuziki mashuhuri nchini alikuwa ameyafunga madarasa matano aliyokarabati akilalamikia kutolipwa shilingi milioni 3.4.

Muhtasari

•Barasa alipigwa na butwaa wakati alienda kuzindua madarasa hayo na kupata kuwa yalikuwa yamefungwa kwa kifuliali na hapo ndipo ghadhabu ikamshinikiza kumshambulia mwanakandarasi Stephen Masinde. 

•Barasa alisema kuwa mkanganyiko uliibuka wakati alienda kumuarifu Masinde afunge zipu ya suruali yake kwani kulingana na yeye ilikuwa wazi.

Image: HISANI

Vurumai ilitanda katika shule ya msingi ya Lurare Baptist iliyo katika eneo bunge la Kimilili baada ya mbunge wa eneo hilo Didmus Barasa kumzaba kofi mwanakandarasi aliyekuwa amepatiwa kazi ya kukarabati madarasa shuleni humo.

Barasa ambaye ni mwandani wa naibu rais William Ruto alipigwa na butwaa wakati alienda kuzindua madarasa hayo na kupata kuwa yalikuwa yamefungwa kwa kifuliali na hapo ndipo ghadhabu ikamshinikiza kumshambulia mwanakandarasi Stephen Masinde. 

Masinde ambaye pia ni mwanamuziki mashuhuri nchini alikuwa ameyafunga madarasa matano aliyokarabati akilalamikia kutolipwa shilingi milioni 3.4.

Video ya mbunge Barasa ilienezwa sana mitandaoni huku Wakenya wakitoa maoni mbalimbali kufuatia tukio hilo.

Masaa machache baadae mbunge huyo alihudhuria mkutano mwingine katika shule ya msingi ya Namasanda na alipokuwa anahutubia waliohudhuria akachukua nafasi ile kutoa simulizi yake kuhusiana na yaliyojiri.

Barasa alisema kuwa mkanganyiko uliibuka wakati alienda kumuarifu Masinde afunge zipu ya suruali yake kwani kulingana na yeye ilikuwa wazi.

"Nilikuwa ninamwambia afunge duka." Mbunge Didmus Baraza atoa sababu ya kumzaba kofi mwanakandarasi. 🎥 : hisani #OngeaUsikike

Posted by Radio Jambo on Saturday, July 31, 2021

Alisema kuwa alipokuwa anaenda kwambia mwanamuziki huyo afunge zipu punde alipomuona alianza kutoroka akidhani kuwa alitaka kumpiga.

"..Kijana mwenyewe akakuja. Alafu kwa vile yeye ni rafiki yangu nikaona sijui alienda kujisaidia na alikuwa hajafunga zipu. Mimi naona gari yake ndogo iko ndani hajafunga nikasema wacha nikimbie nimwambie gereji yako iko wazi funga zipu! Funga duka! Sasa wakati nilifika pale kumwambia namna hivi akatoroka mbio akadhani nataka kumpiga" Barasa alisema.

Alisema kuwa mwanamuziki huyo alishindwa kutegua ishara alizojaribu kumwonyesha kuwa zipu yake ilikuwa wazi.

Barasa pia alikashifu kitendo cha mwanakandarasi huyo kufunga madarasa hayo akidai kuwa wanafunzi walilazimika kukaa nje baada ya Masinde kuwatoa ndani ya madarasa na kuyafunga.