"Imebaki kidogo atembee" mbunge Babu Owino atoa taarifa kuhusu hali ya afya ya DJ Evolve aliyepiga risasi

Kufuatia hayo Evolve alilazwa hospitalini kwa kipindi kirefu na baadhi ya viungo vyake kulemaa.

Muhtasari

•Owino ambaye anahudumu bungeni kwa muhula wake wa kwanza amesema kuwa Orinda anaendelea vyema na matibabu na huenda akaweza kutembea tena hivi karibuni.

•Mwezi Januari mwaka uliopita video ya CCTV iliyomuonyesha mwanasiasa huyo akihusika kwenye mzozo na DJ Evolve wakiwa kwenye kilabu na kisha kumpiga risasi ilienea sana mitandaoni na kwenye vyombo vya habari.

Babu Owino na DJ Evolve
Babu Owino na DJ Evolve

Takriban miezi 19 baada ya mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kumpiga risasi mcheza santuri Felix Orinda almaarufu kama DJ Evolve katika kilabu moja jijini Nairobi, mwanasiasa huyo ametoa taarifa kuhusu hali ya afya ya mhasiriwa.

Owino ambaye anahudumu bungeni kwa muhula wake wa kwanza amesema kuwa Orinda anaendelea vyema na matibabu na huenda akaweza kutembea tena hivi karibuni.

Mwanasiasa huyo alikuwa anamjibu mfuasi wake mmoja kwenye mtandao wa Facebook aliyemwagiza kumuombea Orinda apate afueni ya haraka.

"Ombea DJ uliyepiga risasi pia apone haraka! Jumapili njema mheshiwa" mtumizi wa Facebook aliyejitambulisha kama Conrad Ondari alimwambia Babu.

Mbunge huyo ambaye ni mfuasi mkubwa wa kinara wa ODM Raila Odinga hakusita kumfahamisha mfuasi huyo kuhusu hali ya afya ya DJ Evolve.

"Anaendelea vizuri. Imebaki kidogo tu atembee" Owino alimjibu.

Chapisho la mwanasiasa huyo kwenye ukurasa wake wa Facebook siku ya Jumapili akiwaomba wanaoeneza uvumi kumhusu kumuombea awe mtakatifu kama wao liliibua hisia mbalimbali miongoni mwa wanamitandao wengine wao wakimwagiza kumkumbuka msanii aliyepiga risasi mapema mwaka uliopita katika B-Club.

Mwezi Januari mwaka uliopita video ya CCTV iliyomuonyesha mwanasiasa huyo akihusika kwenye mzozo na DJ Evolve wakiwa kwenye kilabu na kisha kumpiga risasi ilienea sana mitandaoni na kwenye vyombo vya habari.

Kufuatia hayo Evolve alilazwa hospitalini kwa kipindi kirefu na baadhi ya viungo vyake kulemaa. Babu naye alikamatwa ila akawachiliwa siku chache baadae.

Mwezi Juni uvumi ulikuwa umetanda nchini kuwa mcheza santuri huyo alikuwa ameaga dunia kufuatia madhara aliyougua baada ya kupigwa risasi,madai ambayo yalipuuziliwa mbali na familia yake.