Ruto atashinda Raila saa nne asubuhi- Miguna adai

Amedai kuwa kamwe hajawahi kukosea kuhusiana na masuala ya mikakati ya siasa

Muhtasari

•Miguna Miguna amesisitiza kuwa naibu rais William Ruto atamshinda Raila kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

•Miguna amesifia ujuzi wake wa masuala ya siasa na kudai kuwa ndiyo sababu kuu kiongozi wa ODM alimuomba awe mshauri wake kwa kipindi cha mwongo mmoja.

Screenshot_from_2019_12_16_04_21_56__1576488144_66205
Screenshot_from_2019_12_16_04_21_56__1576488144_66205

Aliyekuwa mshauri wa Kisiasa wa kinara wa ODM Raila Odinga, Dkt Miguna Miguna amesisitiza kuwa naibu rais William Ruto atamshinda Raila kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, wakili huyo ambaye kwa sasa anaishi Canada baada ya kufurushwa nchini miaka minne iliyopita amedai kuwa  Ruto atamshinda Raila mapema sana ifikapo siku ya uchaguzi.

"Fahamu kuwa William Ruto atashinda Raila saa nne asubuhi" Aliandika Miguna.

Mkosoaji huyo wa serikali amejipiga kifua na kudai kuwa kamwe hajawahi kukosea kuhusiana na suala la mikakati ya siasa.

Miguna amesema kuwa utaalam wake kuhusiana na masuala ya kisiasa ndio umekuwa tishio kubwa kwa wanasiasa wengi ikiwemo rais wa zamani Daniel Moi na rais Uhuru Kenyatta.

Isitoshe, Miguna amesifia ujuzi wake wa masuala ya siasa na kudai kuwa ndiyo sababu kuu kiongozi wa ODM alimuomba awe mshauri wake kwa kipindi cha mwongo mmoja.

"Sijawahi kukosea kuhusiana na mikakati ya siasa. Ndio maana Moi alinifurusha nchini mwaka wa 1987 na Raila Odinga akanibembeleza niwe mshauri wake kati ya mwaka wa 2006 na 2017. Ndio sababu Uhuru Kenyatta ananiogopa sana hadi ananipatia onyo" Miguna alisema.

Mwaka wa 2017 Miguna alimsaidia Raila kujiapisha kama rais wa watu baada ya IEBC kutangaza Uhuru Kenyatta kama rais wa Kenya .