Jamaa aliyeua mkewe kwa kumkata koo apigwa kitutu hadi kifo Thika, mtoto wa miezi 4 aachwa ndani ya gari

Muhtasari

•Jamaa huyo anadaiwa kutekeleza unyama huo kisha kutoweka na kuacha mtoto wao wa miezi minne kwenye kiti cha dereva..

Crime scene
Crime scene

Jamaa mmoja alipigwa kitutu na kuuawa na wakazi wa maeneo ya Gatuanyaga, Thika kufuatia madai kuwa aliua mkewe kwa kumkata koo ndani ya gari ambalo walikuwa wamekodishwa.

Jamaa huyo anadaiwa kutekeleza unyama huo kisha kutoweka na kuacha mtoto wao wa miezi minne kwenye kiti cha dereva..

Wakazi ambao walikuwa katika ziara yao waliona mahali gari lile lilikuwa limeachwa  na kupata mwili wa mwanamke pale ndani. Hapo wakaanza harakati za kuwinda mshukiwa baada ya kushuku kuwa kuna kitu kibaya kilikuwa kimeendelea pale.

Mashahidi wamesema kuwa wakazi wenye ghadhabu waliwasha moto mkubwa kwenye shamba ambalo mshukiwa alikuwa amejificha ili kumtoa mafichoni na baada ya kumkamata wakampiga hadi akaaga.

Inadaiwa kuwa mshukiwa alikuwa amejaribu kushambulia baadhi ya wakazi ila akalemewa nguvu kwa kuwa walikuwa wengi.

Naibu OCPD wa Thika amesema kwamba jamaa wa karibu wa wawili hao aliwaarifu kuwa walikuwa wapenzi na hata walikuwa wamepata mtoto pamoja.

Inaaminika kuwa jamaa huyo alimdanganya mpenzi wake waende katika eneo hilo fiche wakajivinjari akiwa na nia ya kutekeleza unyama huo.

Bado haijabainika wazi kilichotokea kati yao ambacho kilisababisha mzozo ulioleta maafa. Miili yao inahifadhiwa katika chumba kimoja cha kuhifadhi maiti mjini Thika.