IPOA yaanza uchunguzi wa kifo cha kijana wa miaka 17 anayedaiwa kupigwa risasi na polisi Huruma

Muhtasari

•Maafisa wa IPOA wanatazamia kukusanya ushahidi muhimu kutoka kwa wahusika ikiwemo maafisa wa polisi ili kupata majibu kuhusiana na kifo cha Haila Asanake.

•Polisi walisema kuwa marehemu alipatwa na risasi ambayo ilipigwa hewani na afisa mmoja aliyekuwa na nia ya kutawanya kikundi cha raia ambao walikuwa wanawatupia mawe.

•Mashahidi walidai kwamba  Asanake alikuwa amesimama kwenye roshani ya nyumba yao iliyo kwenye ghorofa ya tatu wakati risasi ilimpata kifuani.

HISANI
HISANI
Image: Marehemu Haila Asanake anayedaiwa kupigwa risasi na polisi

Shirika huru la uangalizi wa polisi nchini(IPOA) linachunguza kifo cha kijana wa miaka 17 anayedaiwa kupigwa risasi na mmoja wa maafisa wa polisi ambao walikuwa wanafanya msako wa madawa ya kulevya  katika mtaa wa Huruma, Nairobi mnamo Septemba 8.

Maafisa wa IPOA wanatazamia kukusanya ushahidi muhimu kutoka kwa wahusika ikiwemo maafisa wa polisi ili kupata majibu kuhusiana na kifo cha Haila Asanake.

Upasuaji wa mwili ambao ulifanya kufuatia kifo chake ulidhihirisha kuwa kijana huyo aliangamia kutokana na kuvunja damu nyingi baada ya kupigwa risasi kwenye kifua chake.

Mwenyekiti wa  IPOA Anne Makori amesisitiza kwamba iwapo yeyote atapatikana na hatia shirika hilo halitasita kutoa mapendekezo ya hatua itakayochukuliwa ikiwemo uwezekano wa kushtakiwa.

Polisi walisema kuwa marehemu alipatwa na risasi ambayo ilipigwa hewani na afisa mmoja aliyekuwa na nia ya kutawanya kikundi cha raia ambao walikuwa wanawatupia mawe.

Mashahidi walidai kwamba  Asanake alikuwa amesimama kwenye roshani ya nyumba yao iliyo kwenye ghorofa ya tatu wakati risasi ilimpata kifuani.

Polisi walieleza kuwa walikuwa wamesimamisha gari ambalo walishuku kutumika na muuzaji madawa ya kulevya  mida ya saa kumi na mbili jioni wakati walikabiliwa na upinzani.

Kizaazaa kilianza na kuvutia baadhi ya wakazi ambao walianza kuwatupia maafisa wale mawe na bidhaa zingine.

Hapo wakalazimika kupiga risasi hewani ili kuwafukuza wakazi wale ambao walitaka mshukiwa aachiliwe huru.

Katika harakati hiyo Asanake akapatwa na risasi moja ila maafisa wale walipokuwa wanaondoka hawakufahamu kuwa kuna mtu aliyekuwa amepatwa na risasi yao.