Mwanafunzi wa darasa la 7 ajitia kitanzi Siaya baada ya kulalamika kuhusu kupigwa na mwalimu mara kwa mara

Alisema kuwa alikuwa amechoshwa na kitendo cha mwalimu huyo.

Muhtasari

•Inasemekana kuwa mvulana huyo alifariki alipokuwa anapokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Siaya baada ya wanafamilia kumpata akiwa ananing'inia kwa mti mmoja nyumbani kwao.

•Dada ya marehemu, Millicent Onyango alisema kuwa ndugu yake alikuja nyumbani akiwa analalamika kwamba kuna mwalimu alikuwa na mazoea ya kumpiga mara kwa mara. Alisema kuwa alikuwa amechoshwa na kitendo cha mwalimu huyo.

meru
meru

Habari na Philip Onyango (KNA)

Wazazi wa wanafunzi wa shule ya msingi ya Kalenjuok, iliyo eneo la Alego kaunti ya Siaya walishiriki maandamano siku ya Jumatano baada ya mmoja wao kujitia kitanzi kutokana na matatizo shuleni.

Evans Onyango ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba anaripotiwa kujitoa uhai mnamo Jumanne jioni muda mfupi tu baada ya kusikika akilalamika kuhusu kupigwa mara kwa mara na mmoja wa walimu wake.

Inasemekana kuwa mvulana huyo alifariki alipokuwa anapokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Siaya baada ya wanafamilia kumpata akiwa ananing'inia kwa mti mmoja nyumbani kwao.

Dada ya marehemu, Millicent Onyango alisema kuwa ndugu yake alikuja nyumbani akiwa analalamika kwamba kuna mwalimu alikuwa na mazoea ya kumpiga mara kwa mara. Alisema kuwa alikuwa amechoshwa na kitendo cha mwalimu huyo.

Millicent alitoka nyumbani na kuacha ndugu yake akiwa amejawa na ghadhabu na baadae mpwa  wao akamuona kwa mti akiwa amejitia kitanzi.

Habari hizo zilipofika shuleni asubuhi ya Jumatano, wanafunzi na wazazi waliokuwa wamejawa na hasira walishiriki maandamano wakilalamikia mwalimu anayedaiwa kusukuma mwanafunzi huyo afike hatua ya kujitoa uhai.

Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Siaya huku upasuaji wa mwili ukisubiriwa.