Mwanamke anusuriwa baada ya mumewe na mwanawe kujaribu kumteketeza kwa madai ya uchawi Makueni

Muhtasari

•Baada ya polisi kumchukua mhasiriwa, mumewe alihamasisha kikundi cha watu kuvamia kituo cha polisi ili kumtoa ila maafisa waliokuwa wanamzuilia wakawafurusha.

crime scene 1
crime scene 1

Mwanamke mmoja kutoka eneo la Kathonweni kaunti ya Makueni alinusurika kifo baada ya kuokolewa na polisi wakati mumewe na mwanawe walijaribu kumteketeza kwa madai kuwa yeye ni mchawi.

Katua Ngudo na mwanawe Ngudo Katua  wanaripotiwa kuteketeza nyumba ya mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 63 siku ya Ijumaa mida ya saa kumi na moja jioni.

Kipande cha nyumba ya mwanawe mhasiriwa Mutinda Katua pia kilichomeka katika harakati za kumwangamiza  ikidaiwa kwamba alikuwa anaendeleza shughuli za uchawi.

Polisi kutoka kituo cha Mavindini walipopokea ripoti walikimbia katika eneo la tukio na kumuokoa mwanamke huyo kisha kuenda naye hadi kituoni.

Baada ya polisi kumchukua mhasiriwa, mumewe alihamasisha kikundi cha watu kuvamia kituo cha polisi ili kumtoa ila maafisa waliokuwa wanamzuilia wakawafurusha.

Kamanda wa polisi katika kaunti ya Makueni Joseph Ole Naipeyan alisema kwamba watu waliohusika kwenye uvamizi wa kituo walikimbia eneo la tukio na juhudi za kuwasaka na kuwatia mbaroni zimeng'oa nanga.

Mhasiriwa alipelekwa katika hospitali ya Kathonzweni ili kutibiwa majeraha ambayo alikuwa amepata.