Jamaa atiwa mbaroni kwa kuua sahibu wake kwa kumdunga kisu kufuatia mzozo wa nauli Kiambu

Muhtasari

•Daniel Waithera (25) anasemekana kumdunga Michael Mukami (21) shingoni kisha kutoweka baada ya kuzozana kuhusu nauli ya pikipiki.

•Baada ya kuwa mafichoni kwa masaa machache hatimaye polisi waliweza kumkamata mshukiwa na kumzuilia kituoni huku akisubiri kufikishwa mahakamani.

Crime scene
Crime scene

Jamaa mmoja anayedaiwa kuua rafiki yake kwa kumdunga kisu katika eneo la Muthangari, kaunti ya Kiambu  ametiwa mbaroni.

Daniel Waithera (25) anasemekana kumdunga Michael Mukami (21) shingoni kisha kutoweka baada ya kuzozana kuhusu nauli ya pikipiki.

Kulingana na DCI, mwendesha pikipiki aliyetambulishwa kama Stephen Mwango alikuwa amewabeba wawili hao kutoka soko ya Gikambura kuwapeleka Muthangari ila walipofika wakaanza kubishana kuhusu nani alifaa kulipa nauli kwa huduma ambayo walipokea.

Baada ya kizaazaa cha muda mfupi mshukiwa anaripotiwa kuelekea kwa nyumba yake na kuchukua kisu chenye makali ambacho alitumia kudunga mwenzake shingoni bila kubisha na kumuacha akiwa hali mahututi

Mwendesha pikipiki ambaye alishuhudia tukio hilo lote alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Kikuyu na juhudi za kuwinda mshukiwa zikang'oa nanga.

Baada ya kuwa mafichoni kwa masaa machache hatimaye polisi waliweza kumkamata mshukiwa na kumzuilia kituoni huku akisubiri kufikishwa mahakamani.

Kisu ambacho kilitumika kutekeleza mauaji hayo pia kilipatikana na kitatumika kama ushahidi kortini.