Jamaa augua majeraha mabaya baada ya kuruka kutoka ghorofa ya 3 ili kuepuka kukamatwa na polisi Embakasi

Muhtasari

•Katika jaribio la kuhadaa maafisa wale, Mongare alizuka kutoka chumba chake cha malazi akiwa uchi wa  mnyama ili apatiwe nafasi ya kuvaa nguo ila kumbe alitaka muda wa kufikiria hatua ambayo angechukua ili asikamatwe.

• Jaribio lake la kuepuka mkono mrefu wa serikali ziliangulia patupu kwani alishindwa kusimama tena baada ya baadhi ya viungo vyake kuvunjika.

crime scene
crime scene

Jamaa mmoja anahudumiwa hospitalini akiwa katika hali mahututi baada ya kuruka kutoka ghorofa ya tatu ya jengo ambalo anaishi ili kuepuka kukamatwa na polisi.

Didmus Mong'are amelazwa katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki baada ya kuugua majeraha mabaya mwilini na baadhi ya viungo vyake kuvunjika aliporuka kutoka kwa roshani ya chumba chake kilicho katika ghorofa ya tatu ya jengo la Amani, mtaa wa Embakasi.

Cha kushangaza ni kwamba maafisa wa polisi ambao alikuwa anatorokea ili wasimkamate ndio walimchukua na kumpatia huduma ya kwanza kabla ya kumkimbiza hospitalini.

Kulingana na DCI, maafisa wawili kutoka kituo cha polisi  cha Embakasi walivamia chumba cha mshukiwa ili kumkamata kwa kupokea pesa kwa njia ya ulaghai.

Katika jaribio la kuhadaa maafisa wale, Mongare alizuka kutoka chumba chake cha malazi akiwa uchi wa  mnyama ili apatiwe nafasi ya kuvaa nguo ila kumbe alitaka muda wa kufikiria hatua ambayo angechukua ili asikamatwe.

Mongare alipomaliza kuvaa suruali na shati alitokea upande wa jikoni kisha akaruka kutoka kwa roshani akitumai kufika chini salama na kutimua mbio.

Hata hivyo jaribio lake la kuepuka mkono mrefu wa serikali ziliangulia patupu kwani alishindwa kusimama tena baada ya baadhi ya viungo vyake kuvunjika.

Mshukiwa atashtakiwa kwa kosa la ulaghai punde atakapopewa ruhusa kutoka hospitalini.