Jamaa amuua mpenzi wake,ajisalimisha kwa polisi

Muhtasari
  • Jamaa amuua mpenzi wake,ajisalimisha kwa polisi
Pingu
Image: Radio Jambo

Wapelelezi wa DCI walioko Kapenguria, wanaandaa mashtaka ya mauaji dhidi ya mshukiwa aliyemuua mpenzi wake na kujisalimisha kwa maafisa Jumatano.

Nelson Baraza, 29, almaarufu ‘TupaTupa’, alitembea kwa kawaida hadi kituo cha Polisi cha Kapenguria katika kaunti ya Pokot Magharibi, na akaomba kuonana na DCIO juu ya jambo ambalo alitaka kuripoti.

Bosi wa DCI George Kinoti alisema kwamba aliongozwa kwa ofisi ya upelelezi wa jinai ambapo aliwaambia maafisa kwamba alikuwa amemuua mpenzi wake na hakutaka jamaa na maafisa wake watumie wakati muhimu kumtafuta.

Kwa hivyo aliwaomba maafisa kuandamana naye hadi mahali alipofanya uhalifu huo na kuacha mwili.

Kinoti aliongeza kuwa maafisa hao, ambao walishangazwa na kukiri kwa mtu huyo, walimhoji zaidi juu ya ukweli wa madai yake, kwani udhibitisho kama huo ni ngumu kupatikana.

Lakini mtu huyo alionyesha ujasiri mwingi katika madai yake, na kusababisha wapelelezi kuandamana naye kwenye eneo la mauaji.

"Baada ya kuwasili chini ya milima wa Kamatira, kilometometri 10 mbali na kituo hicho, walikumbana na mwili wa Egla Chepkorir wa miaka 20, akiwa amejilaza chini ya mti katikati ya shamba la mahindi," Kinoti alisema.

Baraza aliwaelezea wapelelezi kwamba alimuua Egla baada ya kugundua kuwa alikuwa katika mapenzi ya siri na mwanaume mwingine.

Kwa uchungu wa usaliti ambao hauwezi kustahimili, alimshawishi kwenda shamba na akamuua kinyama akitumia leso kabla ya kwenda kituo cha polisi kujiandikisha kwa mauaji.

Maafisa wa Kapenguria walishughulikia eneo la mauaji, walipata leso iliyotumika kumuua mwathiriwa na kumkamata Baraza kwa uhalifu uliokiriwa mwenyewe.