Mshukiwa wa wizi aliyeruka ndani ya choo ili kuepuka kupigwa kitutu ateketezwa akiwa ndani Muranga

Muhtasari

•Kulingana na DCI, Joseph Karanja (30) alikuwa ameiba usiku wa Jumanne kisha kuenda mafichoni baada ya kujulikana.

•Karanja kuona kapatikana aliamua kuruka ndani ya choo cha shimo chenye kina cha futi kumi akiwa na nia ya kuokoa maisha yake

•Mahali alikodhani ni salama paligeuka kuwa kichinjio chake kwani aliteketea hadi kifo akiwa mle ndani.

Image: TWITTER// DCI

Mshukiwa mmoja wa wizi alikumbana na kifo cha uchungu  asubuhi ya Jumatano baada ya kuteketezwa akiwa ndani ya choo cha shimo katika maeneo ya Gatanga, kaunti ya Murang'a.

Kulingana na DCI, Joseph Karanja (30) alikuwa ameiba usiku wa Jumanne kisha kuenda mafichoni baada ya kujulikana.

Juhudi za kuwinda mhalifu yule ziling'a nanga asubuhi ya Jumatano huku wakazi ambao walikuwa wamechoshwa na ongezeko la matukio ya wizi wakijitolea juu chini kuhakikisha wamemnasa mshukiwa.

Baada ya jitihada za muda, wakazi wale waliweza kumuona Karanja akiwa amejificha karibu na nyumbani kwa babake mwendo wa saa nne asubuhi.

Karanja kuona  kapatikana aliamua kuruka ndani ya choo cha shimo chenye kina cha futi kumi akiwa na nia ya kuokoa maisha yake.

Wakazi ambao walikuwa wamejawa na ghadhabu walitafuta kuni  na vifaa vingine ambavyo vinaweza kuwaka na kuzitupa ndani ya shimo ile kisha kuiteketeza.

Mahali alikodhani ni salama paligeuka kuwa kichinjio chake kwani aliteketea hadi kifo akiwa mle ndani.

Hata hivyo, maafisa wa DCI wameonya raia dhidi ya kuchukua sheria mkononi na kuwaagiza kupiga ripoti kila wakati ambapo matukio ya uhalifu yanatokea mahali.