Mudavadi, Kalonzo waapa kufanya kazi na Gideon Moi kuiunganisha Kenya

Muhtasari
  • Mudavadi, Kalonzo waapa kufanya kazi na Gideon Moi kuiunganisha Kenya
Image: Hisani

Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka wameapa kushirikiana na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi, kuiunganisha nchi.

Viongozi hao wawili ambao ni sehemu ya Muungano wa One Ke nya Alliance walizungumza Alhamisi, huko Bomas of Kenya baada ya Gideon kuidhinishwa na chama cha uhuru kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Kulingana na Mudavadi, msimamo ambao Kanu amechukua juu ya maswala yanayoathiri nchi hiyo ndio watakaofuata katika azma ya kuunganisha na kuiendeleza Kenya.

"Hotuba ya Gideon ni hotuba ambayo inalenga mbele, inazungumza kuhusu shida za wakenya, kupigana na ufisadi, elimu, maisha ambayo ni haba kwa wakenya na mimi nasimama naye tukisema tuko tayari kushikana mikono tuweke wakenya mbele na sisi tufuate. Tutazidi, kuongea, kushauriana na kujadiliana… lengo letu ni Kenya inawiri."

Kalonzo alisema kuwa atatembea safari waliyoanza chini ya OKA na Gideon, akiongeza kuwa muungano huo ni mfano wa kupeana mikono kwani umewaleta viongozi kadhaa pamoja.

Alimhakikishia seneta wa Baringo kwamba atashikamana naye hata kama kila mtu ataacha muungano kwa sababu anajua Gideon atamfanyia vivyo hivyo.

"Tufungue macho, safari imeanza," Kalonzo alisema.

Wakuu wa OKA pia walimpongeza Gideon kwa kujiunga na kilabu cha viongozi ambao wameteuliwa na vyama vyao kuwa washika bendera zao za urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao.