Unyama! Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Laikipia auawa kwa kisu na mpenzi wa mwenzake

Muhtasari

•Gertrude Chepkoech ambaye alikuwa katika mwaka wake wa kwanza alifariki kutokana na majeraha mabaya ya kisu mwilini kufuatia tukio ambalo lilitokea mida ya alasiri siku ya Jumatano.

•Baada ya kutekeleza kitendo hicho cha unyama, mshukiwa ambaye alitambulishwa kama Ezra anaripotiwa kujaribu kujitoa uhai pia kwa kujikata koo na kujidunga tumboni. 

Image: HISANI

Habari na KNA/Jesse Mwitua

Hali ya majonzi imetanda katika chuo kikuu cha Laikipia baada ya mwanafunzi mmoja wa kike kuuawa kwa kudungwa kisu na jamaa anayedaiwa kuwa mpenzi wa msichana ambaye wamekuwa wakiishi naye katika chumba kimoja.

Gertrude Chepkoech ambaye alikuwa katika mwaka wake wa kwanza alifariki kutokana na majeraha mabaya ya kisu mwilini kufuatia tukio ambalo lilitokea mida ya alasiri siku ya Jumatano.

Baada ya kutekeleza kitendo hicho cha unyama, mshukiwa ambaye alitambulishwa kama Ezra anaripotiwa kujaribu kujitoa uhai pia kwa kujikata koo na kujidunga tumboni. 

Mmoja wa wafanyikazi katika hosteli ambako marehemu amekuwa akiiishi, Bi Lucy Nakaridi alisema kwamba mshukiwa alikuwa amesafiri kutoka Nakuru kuja kutembelea mpenzi wake ila mzozo ukatokea kati yao hadi ikalazimu usimamizi wa hosteli na majirani kuingilia kati.

Bi Nakiridi alisema kuwa msichana aliyekuwa ametembelewa alilamika kwamba mshukiwa alikuwa anajilazimisha kwake na kufuatia hayo ikabidi amefukuzwa pale.

Baada ya kufukuzwa inadaiwa kwamba jamaa hakuonekana pale tena hadi siku ya Jumatano ambapo alirudi na kuingia katika chumba cha mpenzi wake na kumpata Chepkoech pekee. Kwa wakati huo mpenzi wake alikuwa ameondoka kuenda kufanya mtihani shuleni.

Muda mfupi baada ya Ezra kuingia kwenye hosteli zile majirani waliskia mayowe makali kutoka kwa chumba kimoja na kukimbia pale kuona kilichokuwa kinaendelea.

Jirani mmoja aliyejitambulisha kama Reuben Rendile alisema kwamba walipata mwili wa msichana ukiwa umelala sakafuni. 

Bw. Rendille alisema kwamba mshukiwa alipowaona alijaribu kujitoa uhai kwa kujidunga kisu kwenye tumbo na kujikata koo.

Majirani ambao walifika kwenye eneo la tukio walimshambulia mshukiwa na kumpiga kitutu kutokana na ghadhabu ya unyama ambao mshukiwa alikuwa amefanya.

Polisi walipofika kwenye eneo la tukio walimpata mshukiwa akiwa katika hali mahututi na kumkimbiza katika hospitali ya Nyahururu.

Mwili wa marehemu Chepkoech ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya Nyahururu huku mshukiwa akiendelea  kutibiwa majeraha hospitalini.