Mshtuko Nanyuki baada ya vijana wawili kujitia kitanzi

Wawili hao hawakuacha ujumbe wowote kwa hivyo ni ngumu kubaini kilichowachochea kujitoa uhai

Muhtasari

•Kesi za watu kujitoa uhai zimekithiri sana katika eneo hilo, kesi mbili za hivi karibuni zikifikisha jumla ya waliojitoa uhai ndani ya wiki moja kuwa watu saba

•Chifu amesihi vijana kufunguka kuhusu masaibu yao kwa marafiki, maafisa na wataalam badala ya kufanya maamuzi ya kujitoa uhai.

meru
meru

Hali ya mshtuko imetanda katika eneo la Nanyuki baada ya vijana wawili kupatikana wakiwa wamejitia kitanzi siku ya Jumatatu.

Alipokuwa anathibitisha matukio hayo, chifu wa Nanyuki Duncan Wachira alisema kuwa jamaa wale walijitoa uhai katika sehemu mbalimbali za mji huo asubuhi ya Jumatatu. Wachira alisema kwamba wawili hao hawakuweza kutambulishwa mara moja.

Mwili mmoja ulipatikana ukiwa umening'inia kwa mti mmoja katika makaburi  ya Waislamu, eneo la Asian Quarters ilhali mwili wa pili ulipatikana ndani ya chumba cha kukodishwa upande wa Thingithu.

Wachira alisema kuwa kesi za watu kujitoa uhai zimekithiri sana katika eneo hilo, kesi mbili za hivi karibuni zikifikisha jumla ya waliojitoa uhai ndani ya wiki moja kuwa watu saba.

"Hawa vijana wote ambao wamejitoa uhai katika kipindi cha wiki moja illiyopita hawajatimia umriwa miaka 35. Inashtua matukio haya kutokea ndani ya wiki moja" Wachira alisema.

Alisema kwamba alipokea simu asubuhi ya Jumatatu kutoka kwa mzee mmoja wa Nyumba Kumi ambaye alimfahamisha kuhusu jamaa ambaye alikuwa amejitoa uhai katika eneo la Asian Quarters. 

Majina ya marehemu hayakutambulishwa kwani familia zao hazikuwa zimefahamishwa. Wawili hao hawakuacha ujumbe wowote kwa hivyo ni ngumu kubaini kilichowachochea kujitoa uhai.

Chifu amesihi vijana kufunguka kuhusu masaibu yao kwa marafiki, maafisa na wataalam badala ya kufanya maamuzi ya kujitoa uhai.