Jamaa aua mkewe kwa kumdunga kisu moyoni kisha kujaribu kujitoa uhai kwa kuruka kutoka ghorofa ya 4 Nakuru

Muhtasari

•Juhudi za jamaa huyo za kujaribu kuepuka matokeo ya matendo yake ziliangulia patupu kwani hakufariki baada ya kuanguka chini ila aliumia vibaya kwenye miguu yake na kushindwa kuamka

crime scene 1
crime scene 1

Polisi mjini Nakuru wanazuilia jamaa mmoja anayedaiwa kuua mkewe kwa kudunga kisu kisha kujaribu kujitoa uhai pia bila mafanikio.

Paul Ochieng' anaripotiwa kudunga mkewe, 25, kwenye moyo kufuatia mzozo wa kinyumbani  kisha kuruka kutoka kwa ghorofa ya nne akikusudia kujitoa uhai ili kuepuka kupigwa kitutu na umma ambao ulikuwa umejawa na ghadhabu.

Juhudi za jamaa huyo za kujaribu kuepuka matokeo ya matendo yake ziliangulia patupu kwani hakufariki baada ya kuanguka chini ila aliumia vibaya kwenye miguu yake na kushindwa kuamka.

Kulingana na DCI, majirani wa mshukiwa walipigwa na butwaa kubwa  kuona yaliyokuwa yamejiri na wakafahamisha maafisa wa polissi ambao walifika kwenye eneo la tukio muda mfupi baadae.

Maafisa wale wakiongozwa na kamanda wa polisi katika kaunti ya Nakuru waliweza kupata kisu ambacho mshukiwa  anadaiwa kutumia kutekeleza unyama dhidi ya mkewe.

Mshukiwa alipelekwa katika hospitali ya Nakuru PGH ambako anaendelea kupokea matibabu  chini ya ulinzi mkali wa polisi huku akisubiri kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Jack mjini Nakuru.