Jinsi polisi walivyokamata watu waliokuwa wanachimba visima vya ndoa hadharani wakidhani ni majambazi Ruai

Muhtasari

•Maafisa kutoka kituo kimoja cha Ruai walipokea ripoti kutoka kwa mkazi mmoja kwamba kulikuwa na gari geni ambalo alitialia shaka lililokuwa limeegeshwa karibu na kwake mida ya saa tisa usiku wa kuamkia Ijumaa.

•Gari la washukiwa liliposimama baada ya magurudumu kuishiwa na hewa, maafisa wale waliona watu wanne waliokuwa uchi wa mnyama wakitoka mle ndani huku wakiwa wameinua mikono hewani kuashiria kuwa walikuwa wanajisalimisha kwa amani

crime scene
crime scene

Drama kubwa ilitokea katika eneo la Ruai, kaunti ya Nairobi usiku wa kuamkia Ijumaa baada ya maafisa wa polisi kugundua kwamba washukiwa waliokuwa wamekimbiza kwa ari wakidhani ni wezi hawakuwa majambazi ila kosa lao lilikuwa kufanyia tendo la kitandani pahali pasipofaa.

Maafisa kutoka kituo kimoja cha Ruai walipokea ripoti kutoka kwa mkazi mmoja kwamba kulikuwa na gari geni ambalo alitialia shaka lililokuwa limeegeshwa karibu na kwake mida ya saa tisa usiku na hakufahamu nia ya wenye kuliegesha pale.

Kulingana na DCI, mkazi huyo alihofia kwamba huenda wenye kuegesha gari lile walikuwa na nia mbaya na ndiposa akapiga ripoti.

Polisi walipofika kwenye eneo la tukio waliona watu wanne wakiingia ndani ya gari lile haraka kisha wakaliendesha kwa mwendo wa kasi na kutoweka.

Kwa kuwa maafisa wale walikuwa na hamu ya kufahamu kile ambacho washukiwa wale walikuwa wanafanya walichukua gari lao aina ya Land Cruiser na kuwafuata mbio.

Baada ya kuwakimbiza washukiwa  kwa takriban kilomita tano bila kufanikiwa kuwakamata , maafisa wale waliamua kupiga magurudumu ya gari lao risasi na kulifanya lipunguze kasi.

Gari la washukiwa liliposimama baada ya magurudumu kuishiwa na hewa, maafisa wale waliona watu wanne waliokuwa uchi wa mnyama wakitoka mle ndani huku wakiwa wameinua mikono hewani kuashiria kuwa walikuwa wanajisalimisha kwa amani.

Wanne hao walikuwa wanaume wawili na wanawake wawili. 

Mmoja wa wanawake wale alifahahamisha polisi kwamba wao sio wezi ila kosa lao  tu lilikuwa kula uroda wakiwa pahali pasipofaa.

Polisi walishangaa kugundua kuwa juhudi zao za kukamata majambazi ziliwapelekea kuharibu sherehe ya wanne ambao walikuwa wameamua kupeleka burudani yao barabarani.

Hata hivyo wanne hao walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi pamoja na gari walilokuwa wameabiri.