Polisi katika kaunti ya Kirinyaga wanawasaka wanafunzi 14 ambao waliruka kutoka kwa matatu iliyokuwa inaelekea Nairobi kupitia kwa madirisha baada ya kugundua kwamba dereva alikuwa amebadilisha njia na sasa alikuwa anawapeleka katika kituo cha polisi kuripoti walikuwa wanavuta bangi.
Kulingana na DCI, wanafunzi hao kutoka shule ya sekondari ya Fred's Grammar walikuwa wameabiri matatu ya 2NK Sacco katika kitup cha basi cha Karatina wakielekea nyumbani kwa kipindi cha likizo fupi.
Walipofika eneo la Kibingoti, dereva wa matatu aliyetambulishwa kama John Maina alinusa harufu kali ya mihadarati aina ya bangi kutoka nyuma ya matatu hiyo.
Dereva huyo alipochungulia kwenye kioo cha kando aliona moshi ukitoka midomoni mwa wanafunzi ambao alikuwa amebeba huku wengine wakibugia vileo.
Alijaribu kuwasihi wakome kutumia mihadarati ndani ya gari yake ila wanafunzi wale wakaanza kumtishia na kumuagiza aachane nao na ashughulike na kuendesha gari tu.
Kutokana na ghadhabu iliyokuwa imempata dereva huyo aliamua kubalisha mkondo na kuelekea katika kituo cha polisi cha Sagana kupiga ripoti ila wanafunzi wale walipogundua kilichokuwa kinaendelea wakaanza kuruka mmoja mmoja kupitia kwa dirisha.
Matatu ile ilipofika katika kituo cha polisi hamkuwa na mwanafunzi yeyote ndani ila misokoto ya bangi, chupa za pombe na mizigo ambayo washukiwa walikuwa wameacha nyuma.
Kufuatia hayo wapelelezi kutoka kituo cha Sagana waliita mwalimu mkuu wa shule hiyo ili awasaidie kutambua wanafunzi wahusika.