Wahariri wataka uchunguzi wa haraka kufanyika kuhusu kifo cha wanahabari wawili

Muhtasari
  • Wahariri wataka uchunguzi wa haraka kufanyika kuhusu kifo cha wanahabari wawili

Chama cha Wahariri cha Kenya kimeelezea wasiwasi wake kufuatia hali mbaya ya kifo cha mhariri mkongwe wa sayansi Gatonye Gathura.

Gathura alifanya kazi kama mhariri wa sayansi katika Daily Nation na baadaye kama mwandishi katika Standard.

Ripoti za polisi zinaonyesha kuwa mwili wa mwanahabari huyo ulipatikana Oktoba 26, 2021, Naivasha na umelazwa katika chumba cha kuhifadhi maiti tangu wakati huo.

Katika taarifa, Rais wa Chama cha Wahariri wa Kenya Churchill Otieno alisema kuwa kwa wakati huu, kuna habari chache kuhusu lini na jinsi Gathura aliaga dunia.

Wakati uo huo, Chama pia kimefahamu kuhusu kifo cha ghafla cha Joshua Nanjero wa Standard Group, ambaye alipatikana amekufa nyumbani kwake Nairobi. Nanjero alikuwa mchora katuni wa The Nairobian.

Chama cha Wahariri kinatoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua za haraka ili kubaini ukweli kuhusu vifo hivyo viwili.

Inataka uchunguzi wa haraka wa kesi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho na kutoa mwanga kuhusu mazingira ya vifo hivyo na imemtaka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuamuru uchunguzi ufanyike.

Chama cha Wahariri wa Kenya pia kimetuma risala zake za rambirambi kwa familia na kuwatakia faraja na nguvu, na kinajitolea kusalia imara katika kufanya kila liwezekanalo ili kubaini hali zinazozunguka vifo hivyo viwili.