"Machozi ya siri hutiririka kila tunapokufikiria!" Mike Sonko amkumbuka marehemu mamake kwa ujumbe wa kihisia

Muhtasari

•Sonko ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuadhimisha miaka 24 tangu mama yake, Saumu Mukami Kaimathari Mbuvi alipoaga dunia.

•Amesema kifo cha mama yake kilimdilisha kuwa mtu mwenye huruma huku akieleza maisha yake hayajakuwa rahisi tangu alipompoteza.

Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Gideon Kioko Mbuvi almaarufu kama Mike Sonko amemkumbuka marehemu mama yake ambaye alifariki zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Sonko ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuadhimisha miaka 24 tangu mama yake, Saumu Mukami Kaimathari Mbuvi alipoaga dunia.

Katika ujumbe wake, mwanasiasa huyo amesema ni uchungu sana kupoteza mama na kufichua bado huwa anaumia moyoni kila anapomkumbuka. Amesema kifo cha mamake kilimbadilisha kuwa mtu mwenye huruma huku akieleza maisha yake hayajakuwa rahisi tangu alipompoteza.

"Ni miaka 24 sasa tangu ulipoenda kuwa na Mungu. Nashukuru Mungu kwa muda ambao alitupa sisi watoto wako kukujua na kukupenda. Maisha yako yalinifanya kile nilicho leo na kifo chako kikanifanya kuhisi uchungu wa watu wengine wanaoumia na kuteseka. Machozi ya siri bado hutiririka tunapokufikiria. Kuishi bila wewe ni karibu haiwezekani. Ulipokuwa hai tulikupenda na hata baada ya kufa tunakupenda. Tunashukuru Mungu kwa kuruhusu tuwe sehemu ya maisha yako. Tunajua bado uko nasi  ukituangalia. Kuenda kwako kulibadili maisha yetu kabisa na kutufanya tukupende zaidi" Sonko ameandika.

Amewaombea amani na faraja wale ambao wanaomboleza kwa sasa huku akimtaka mama yake aendelee kupumzika kwa amani.