Dereva John Maina Muthoni anayeripotiwa kupoteza kazi yake baada ya kuripoti kikundi cha wanafunzi wa shule ya upili ambao walikuwa wanavuta bangi na kupiga maji ndani ya matatu ambayo alikuwa anaendesha takriban wiki mbili zilizopita amesimulia yaliyojiri siku hiyo.
Akiwa kwenye mahojiano na Wambui wa Mwangi, Maina ambaye amepongezwa sana kutoka na kitendo chake cha kishujaa alisema wanafunzi wale walichagua kuabiri matatu yake kwa sababu ilikuwa imetengezwa vizuri na kuwekwa muziki.
Alisema wanafunzi wale walikuwa wanaelekea upande wa Nairobi na mwanafunzi wa mwisho angeshukia eneo la By Pass.
"Walikuja wanafunzi 14 wakasema wanataka gari hiyo. Mwenye gari alikuwa ameitengeneza vizuri, ata iko na muziki. Wanafunzi wanapendagari ambayo inacheza muziki. Waliangalia wakaona gari inalipisha 250, wakasema waingie kwa sababu mwanafunzi wa mwisho angeshukia By Pass. Walilipa na wakaandikiwa" Alisema Maina.
Maina alisema baada ya kuendesha kilomita chache kutoka mji wa Karatina alianza kunusa harufu ya bangi ila hakujua ilikuwa inatoka wapi.
Aliendelea na safari yao ila baadaa ya kupiga hatua zingine chache harufu ya pombe ikatanda mle ndani ya gari na hapo ndipo alisimamisha gari na kuwaonya wanafunzi wale dhidi ya kuendelea kutumia mihadarati ile.
"Tulipofika Kibingoti nilinusa harufu ya bangi. Nilidhani ni mtu ambaye alikuwa anatembea ama alikuwa kwa pikipiki alikuwa anavuta. Niliendesha nikiwa makini. Walipofungua pombe harufu pale ndani ya gari ikawa imechanganyika. Nilisimama karibu na mlima nikatoka nikawaambia ningewapeleka kwa polisi" Maina alisimulia.
Alisema mwanafunzi mmoja alimtishia kwamba babake ni mkubwa katika idara ya polisi na angemshtaki kwake ili akamatwe apate adabu.
Isitoshe wanafunzi wengine walimtishia kifo na kufuatia hayo akapatwa na woga mkubwa akarudi kwenye usukani na kuendelea kwa safari ila akabadilisha njia na kuanza kuelekea kituoni.
"Kijana mmoja mfupi aliniambia babake ni mkubwa sana katika idara ya polisi. Alisema ingekuwa vizuri nikiwapeleka kwa polisi kwani ningekaatwa nifungiwe ndani nipate adabu. Wanafunzi hao wengine waliniambia wangeniua. Niliona huenda wakaniangamiza nikapatwa na woga, nikaingia kwa gari ata hawakujua nilifikiria vipi. Walicheka sana. Niliendelea na safari. Baada ya kuvuka matuta ya Sagana kuna kituo cha polisi. Nikienda kuingia pale kulikuwa na msongamano wa magari. Waliona nimegeuza njia wakafungua dirisha wakaanza kutoka. Niliona badala ya kuendelea na safari niwakanyange nikatoka" Alisema.
Alisema muda wa kutoka kwenye kiti chake na kuelekea kwa mlango wa abiria tayari wanafunzi wote walikuwa wameruka na kutoroka.
Wafanyibiashara waliokuwa wanaendeleza shughuli zao za kawaida kando ya barabara walifika mahali matatu hiyo ilikuwa imesimama na kuanza kumhoji Maina kuhusu kilichokuwa kinaendelea.
Alisema aliwakataza dhidi ya kuwakimbiza wanafunzi wale kwani ingemletea shida iwapo ajali ingetokea katika harakati zile.
"Walinionyesha mahali ningepitia kuelekea kwa polisi. Hata sikufunga gari. Nilitoka nikaacha ikiguruma nikaenda kwa afisa. Nilidhani askari wangesema turudi kwa gari tuende tukawasake. Walisema jambo hilo ni hatari kwani wanafunzi wale tayari walikuwa wamevuta bangi na iwapo yeyote angegongwa na gari akikimbia polisi ndiye angekuwa taabani" Alisema.
Alifichua kwamba polisi walipata mifuko sita ya wanafunzi, chupa za pombe na misokoto ya bangi ambayo wanafunzi waliacha nyuma wakati walitoroka.
Baada ya hayo alipigia bosi wake na kumfahamisha kuhusu yaliyokuwa yametokea ila akahisi kama kwamba hakuridhika kusikia habari zile..Siku iliyofuata alipigwa kalamu.