Mwili wa Desmond Tutu walazwa katika kanisa lake la zamani kwa heshima ya kitaifa

Muhtasari

•Mazishi yake rasmi ya kiserikali yatafanyika tarehe 1 Januari baada ya kipindi cha kulazwa, kuruhusu waombolezaji kuupita mwili wake na kuuaga kwa mara ya mwisho.

Image: GETTY IMAGES

Mwili wa Hayati Askofu Mkuu Desmond Tutu umewasili katika Kanisa Kuu la Mtakatifu George mjini Cape Town ambapo utalala kwa siku mbili kwa heshima ya kitaifa.

Tutu, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ambaye alisaidia kukomesha ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, alifariki Jumapili akiwa na umri wa miaka 90.

Mazishi yake rasmi ya kiserikali yatafanyika tarehe 1 Januari baada ya kipindi cha kulazwa, kuruhusu waombolezaji kuupita mwili wake na kuuaga kwa mara ya mwisho.

Umati mkubwa unatarajiwa kuzuru kanisa kuu kwa muda wa siku mbili zijazo.

Muda wa kulazwa katika kanisa hilo ulilazimika kuongezwa hadi siku mbili, "kwa kuhofia kunaweza kutokea mkanyagano," kasisi wa eneo hilo aliliambia shirika la habari la AFP.

Mapadre walichoma uvumba wakati jeneza la Tutu la misonobari likibebwa ndani ya kanisa kuu.

Image: GETTY IMAGES

Mjane wa Tutu Leah alitembea nyuma polepole wakati jeneza likiingia katika parokia yake ya zamani.

Umma utaweza kutoa heshima zao kwa kiongozi huyo wa kidini anayeheshimika sana, nguzo muhimu katika mapambano ya kukomesha mfumo wa ubaguzi wa rangi uliotekelezwa na serikali ya wazungu wachache dhidi ya weusi walio wengi nchini Afrika Kusini kuanzia 1948 hadi 1991.

Ibada za ukumbusho zitafanyika kote Afrika Kusini huku usiku wa karibu wa ukumbusho na marafiki zake wa karibu utafanyika baadaye.

Baada ya mazishi ya Jumamosi, mabaki ya Tutu yatachomwa na majivu yake kuwekwa katika kanisa kuu, ambapo alihubiri kwa miaka mingi.

Kengele za kanisa kuu hilo zimekuwa zikilia kwa dakika 10 kila siku saa sita mchana tangu kifo chake.

Yatakuwa mazishi rahisi kulingana na matakwa yake.

"Hakutaka majivuno au matumizi ya kifahari," wakfu wake ulisema, na kuongeza kuwa hata "aliuliza jeneza liwe la bei nafuu zaidi".