'Bwanangu alioa mwanamke mwingine mnamo siku ya mazishi ya mtoto wetu" Mwanadada asimulia

Muhtasari

•Alisema kwamba mumewe alikosa kuhudhuria  mazishi ya mtoto wao akidai kuwa alikuwa ametiwa mbaroni, madai ambayo alikuja kugundua baadae yalikuwa ya uongo tu.

•Jamaa huyo alimdanganya kwamba alikuwa anaenda ziara ya kibiashara ila ukweli ni kuwa alikuwa anaenda Honeymoon na kipenzi chake kipya.

Image: HISANI

Mwanamke mmoja ameacha wanamitandao wakifuta machozi baada ya kusimulia kisa cha kuhuzunisha kuhusu masaibu aliyopitia mwezi uliopita.

Mwanamke huyo ambaye  kwa sababu zake binafsi hakutaka kutambulishwa alisema mtoto wake wa miaka mitatu aliaga dunia mnamo Desemba 14 kisha wakamzika siku nne baadae.

Alisema kwamba mumewe alikosa kuhudhuria  mazishi ya mtoto wao akidai kuwa alikuwa ametiwa mbaroni, madai ambayo alikuja kugundua baadae yalikuwa ya uongo tu.

"Mtoto wangu wa miaka mitatu alifariki tarehe 14 Disemba. Tuliamua kumzika tarehe 18. Mnamo tarehe 17 nilipigiwa simu nikaarifiwa kuwa mume wangu amekamatwa na aliyenipigia akakata simu kabla sijauliza habari zaidi. Tulimzika mtoto wangu bila yeye. Alikuja tu tarehe 19 na kuniambia ilikuwa kukamatwa kwa makosa" Mwanamke huyo alisimulia.

Baada ya mumewe kurejea nyumbani siku moja baada ya mtoto wao kuzikwa mwanamke huyo alimpeleka hadi walipomzika na wakaomboleza pamoja.

Cha kusikitisha zaidi ni kwamba baadae alipigiwa simu na mpenzi wa zamani wa mumewe akamfichulia kwamba mnamo siku ya mazishi ya mtoto wake, jamaa huyo alikuwa anafunga ndoa na mwanamke mwingine sio eti alikuwa amekamatwa.

Jamaa huyo alimdanganya kwamba alikuwa anaenda ziara ya kibiashara ila ukweli ni kuwa alikuwa anaenda Honeymoon na kipenzi chake kipya.

"Aliniambia alikuwa anaenda ziara ya kikazi kwa siku chache. Siku moja baada yake kuondoka nilipigiwa simu na ex wake akiniambia kuwa siku tulipokuwa tunamzika mtoto wangu,mume wangu kweli alikuwa anafunga ndoa. Ziara ya kikazi aliyoniambia kuhusu ilikuwa ni honeymoon yake. Alimuoa msichana niliyewahi kumuuliza akaniambia ni binamu yake wa mbali. Nilimtumia ujumbe mrefu nikimwambia najua siri yake na niliumia sana" Alisimulia.

Alisema kwamba mumewe jamaa huyo alisita kujibu ujumbe ambao alimtumia licha ya kuusoma.

"Baba yupi anakosa kuhudhuria mazishi ya mwanawe? Uchungu ambao nahisi kwa sasa ni mkubwa. Nimekuwa naye tangu 2016 na alioa mwanamke aliyepatana naye mwezi Juni" Mwanadada huyo alisimulia.