Mkenya wa kwanza mwathirika wa UKIMWI apokea dawa ya HIV

Muhtasari

• Mkenya wa kwanza amepata chanjo dhidi ya Ukimwi miezi 3 baada ya kuidhinishwa na USA na UK.

• Chanjo hiyo ya kudungwa inapeanwa mara moja kila baada ya miezi miwili.

Image: THE STAR

Mwishoni mwa mwezi jana, Kenya ilipiga hatua baada ya Mkenya wa kwanza kupata dawa ama chanjo ya kwanza kabisa dhidi ya virusi vya HIV, miezi mitatu tu baada ya Uingereza na Marekani kutangaza kuidhinisha matumizi ya dawa hiyo ya kujikinga dhidi ya kirusi cha Ukimwi. Dawa hiyo inapeanwa kwa njia ya sindano na wala si vidonge.

Mkenya huyo ambaye jina lake lilibanwa alipokea chanjo hiyo ya antiretroviral therapy (ART) baada ya kupokea mafunzo kwa kina kuhusu matumizi na ufanyaji kazi wa dawa hiyo katika hospitali ya chuo kikuu cha Agha Khan jijini Nairobi.

Dawa hiyo ya ART iliidhinishwa na maabara za Kimarekani na Uingereza baada ya uchunguzi na vipimo vya muda ambapo waliafikia kwamba inaweza kudungwa kwa mtu mzima ambaye ako katika hatari ya kuambikizwa ukimwi au hata na vijana wenye uzani wa kilo 35 kwenda juu.

Chanjo hiyo inadungwa kwa mwili kila baada ya miezi miwili.

Kulingana na ripoti ya wizara ya Afya, inakadiriwa kuwa idadi ya watu wanaoishi na HIV na ambao wanatumia tiba ya kuokoa maisha imeongezeka kutoka 600,000 mwaka 2013 hadi milioni 1.2 mwaka 2021.