Afisa wa polisi taabani kwa kubaka mwanamke ndani ya seli

Muhtasari

•Erick Machuki alikamatwa Jumanne baada ya mwanamke wa miaka 23  kumshtumu kwa kumbaka.

Jail bars
Jail bars
Image: FREEPIK

Afisa mmoja anayefanya kazi katika kituo cha polisi cha Mogotio amejipata matatani baada ya kudaiwa kubaka mwanamke wa miaka 23 ndani ya seli.

Erick Machuki alikamatwa Jumanne baada ya mwanamke wa miaka 23  kumshtumu kwa kumbaka.

Kulingana na ripoti ya polisi, mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo Aprili 27, 2022 mwendo wa saa tatu usiku. Wakati huo mlalamishi alikuwa amezuiliwa pale kwa kosa la kutelekeza mwanawe.

Inasemekana mshukiwa alikuwa ameshika zamu katika eneo la seli wakati alimshambulia mhasiriwa na kumbaka.

Mlalamishi alipiga ripoti kwa afisa wa kike ambaye alichukua usukani asubuhi  baada ya mshukiwa kumaliza zamu yake. 

Punde baada ya mlalamishi kupiga ripoti uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo ulianzishwa na yeye pamoja na mshukiwa wakapelekwa katika hospitali ya Mogotio kwa uchunguzi wa kidaktari.

Mashtaka ya ubakaji yalifunguliwa dhidi ya mshukiwa na faili yake ikakabidhiwa kwa DPP kwa maelekezo zaidi.

Mshukiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi leo. (Jumatano Mei 4, 2022)