Kikosi cha pamoja cha maafisa kutoka vitengo mbalimbali vya polisi wamemtia mbaroni mshukiwa mmoja na kunasa bastola kwenye barabara kuu ya Isiolo-Moyale.
Kulingana na idara ya DCI Abdulahi Hussein Sharamo alikamatwa mapema siku ya Ijumaa katika kizuizi cha polisi na bastola aina ya P29 kupatikana kwake.
Katika ujumbe wake kwenye Twitter DCI ilisema kwamba polisi walikuwa tu wanafanya msako wa kushtukiza kwa abiria wanaotumia barabara hiyo.
Sharamo alikuwa ameabiri basi kulekea Moyale na alikuwa na miraa aliyokuwa amefunga ndani ya jani la mgomba.
Alipokaguliwa alipatikana na bastola ambayo ilikuwa imefichwa ndani ya miraa.
Polisi walipomkagua zaidi walipata risasi mbili zaidi. Mshukiwa ametiwa mbaroni na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Archer katika kaunti ya Samburu.
Taarifa ya DCI ilisema kwamba atafikishwa mahakamani kwa kosa la kuwa na bunduki bila leseni. Uchunguzi pia umeanzishwa kubaini kama bastola hiyo imetumika katika visa vya uhalifu.