"Tulihisi familia yetu imekamilika" Sonko amsherehekea mtoto aliyechukua kulea baada ya mamake kuuawa

Muhtasari

•Satrine Osinya ambaye alichukuliwa na mwanasiasa huyo mwaka wa 2014 baada ya kupoteza mama yake alitimiza miaka 10.

•Sonko amemtakia mwanawe huyo kheri za siku ya kuzaliwa huku akimhakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Mmoja wa watoto ambao gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko anawalea aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa Jumanne.

Satrine Osinya ambaye alichukuliwa na mwanasiasa huyo mwaka wa 2014 baada ya kupoteza mama yake alitimiza miaka 10.

Akisherehekea siku ya kuzaliwa ya Satrine, Sonko alisema ujio wake kwenye maisha yao uliwaletea furaha tele na kufanya wahisi kama kwamba familia yao imekamilika. 

"Ulikuja katika familia yetu miaka 8 iliyopita kama malaika na baraka na tangu wakati huo, tulihisi kwamba familia yetu ilikuwa imekamilika. Wewe ni chanzo cha furaha kwetu na daima tunajihisi kubarikiwa na kuwa na bahati kuwa nawe karibu ukiwa na afya njema na furaha licha ya yale yaliyokupata tarehe 22 Machi-2014 ulipompoteza mama yako mpendwa katika shambulio la kigaidi na kutoroka na majeraha ya  kutisha," Sonko alimwambia Satrine kupitia Facebook.

Sonko alimchukua Satrine pamoja na ndugu yake mkubwa kama watoto wake baada ya mama yao kuuawa kwenye shambulizi la kigaidi lililotokea Machi 2014 katika kanisa moja la eneo la Likoni, kaunti ya Mombasa.

Kaka mkubwa wa Satrine, Gift Osinya ndiye aliyemuokoa kutoka eneo la mashambulizi baada ya mzazi wao kuangamizwa kwa risasi.

Sonko amemtakia mwanawe huyo kheri za siku ya kuzaliwa huku akimhakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Unapofikisha miaka 10 leo, nataka kukutakia heri ya kuzaliwa mtoto Satrine Osinya. Kumbuka nakupenda sana na nakutakia mema kadri unavyozidi kukua," Aliandika.

Mgombea huyo wa ugavana wa Mombasa aliambatanisha ujumbe wake na picha za kumbukumbu za maisha ya Satrine kufikia sasa.