Mhubiri taabani kwa kuchoma miguu ya wavulana watatu kwa madai ya wizi wa keki

Muhtasari

•Mhubiri huyo alikamatwa pamoja na mshukiwa mwingine mmoja kuhusiana na madai ya kuchoma miguu ya wavulana watatu wanaodaiwa kuiba keki.

•Wavulana hao walilia kwa uchungu huku wakiomba kuhurumiwa ila washukiwa walikuwa wametia pamba kwenye masikio yao

Kanisa
Kanisa
Image: BIBLE STUDY TOOLS

Mhubiri  mmoja amejipata taabani baada ya kudaiwa  kutesa vijana watatu kwa kuiba keki katika duka la kuoka mikate mjini Kabarnet, kaunti ya Baringo.

Mhubiri huyo wa kanisa la Deliverance alikamatwa pamoja na mshukiwa mwingine mmoja kuhusiana na madai ya kuchoma miguu ya wavulana watatu wanaodaiwa kuiba keki.

Inaripotiwa kuwa mshukiwa alimpata mmoja kati ya wavulana hao watatu akiiba keki ya thamani ya Ksh 80 ndani ya duka hilo na kufahamisha wafanyikazi ambao walishirikiana naye kuchoma miguu yake kutumia jiko la kuoka mikate.

Huku wakiendelea kumtesa kwa moto washukiwa wanaripotiwa kulazimisha mvulana huyo kufichua majina ya washirika wake katika wizi wa keki.  

Baada ya kupatiwa majina ya wavulana mhubiri huyo aliandamana na wenzake hadi nyumbani kwao na kuwachukua kisha kuwapeleka kwenye duka lile la mikate ambapo walimpitishia mateso kama yale yale waliyofanyia mwenzao.

Wavulana hao walilia kwa uchungu huku wakiomba kuhurumiwa ila washukiwa walikuwa wametia pamba kwenye masikio yao.

Wakazi wa eneo hilo ambao walisikia vilio vya wahasiriwa waliingilia kati na kufahamisha polisi kuhusu yaliyotokea.

Mhubiri huyo na mwenzake walitiwa mbaroni na kupelekwa katika kituo cha polisi huku wakisubiri kufikishwa mahakamani.