Sala ilikuwa inaendelea wakati mlio wa kwanza uliposikika. Kwa makumi ya waumini katika Kanisa Katoliki la St Francis huko Owo, kusini-magharibi mwa Nigeria, sala ya Bwana iligeuka kuwa maombi ya mwisho.
Wanaume waliokuwa na silaha ambao walipenya milango ya kanisa mwendo wa saa 11:30 siku ya Jumapili walirusha baruti iliyosababisha waumini kukimbia kuepuka milipuko hiyo.
Waabudu walipokuwa wakikimbilia njia nyingine mbili za kutokea katika machafuko hayo, walikutana na watu zaidi wenye silaha, na kufuatiwa na risasi zaidi na kishindo kikubwa.
Mwishoni, walioshuhudia wanasema takriban miili 50 - baadhi yao ikiwa ni watoto - iliachwa ikiwa imetapakaa katika sakafu ya kanisa, huku wengine wengi wakijeruhiwa.
Kulikuwa na damu kwenye madhabahu, damu kwenye sakafu, miili kwenye viti.
Bado haijabainika ni watu wangapi wamefariki na au kujeruhiwa. Lakini Askofu wa Jimbo Katoliki la Ondo anasema kanisa hilo ambalo ni mojawapo ya parokia kubwa katika jimbo la Ondo linaweza kubeba hadi watu 1,200. Ilikuwa imejaa wakati wa shambulio hilo.
"Waliua hadi wakaridhika kabla ya kuondoka," mwimbaji wa kwaya John Nwovu aliambia BBC.
Alijificha pamoja na wengine wakati shambulio hilo - ambalo lilidumu kwa takriban dakika 30 - likiendelea na kusema aliokolewa tu kwa neema ya Mungu.
Mlipuko ulilipua dari iliyokuwa juu yake, na kumzika yeye na wengine kadhaa, alisema.
Walibeba uzito na maumivu kimya kimya huku wauaji wakienda huku na huko, wakiwaua waabudu waliokuwa wamejificha chini ya viti.
Kakake Bw Nwovu, ambaye pia ni mwimbaji wa kwaya, alipigwa risasi ya mguu na anaendelea kupata nafuu hospitalini.
"Sidhani mshtuko wa kile nilichokiona utaniacha maisha yangu yote," alisema.
Mabaki ya baruti bado yanatapakaa kanisani, huku chumba cha kuhifadhia nguo - ambako wengi walijificha - kinatoa ushuhuda wa machafuko hayo.
Viatu, kurasa za Biblia zilizolowa damu, mikoba na vitu vingine vya kibinafsi bado vimetawanyika.
Kwa washiriki wa jamii hii tulivu katika jimbo la Ondo, kanisa lilikuwa zaidi ya mahali pa ibada - limekuwa sehemu ya maisha yao tangu kuzaliwa.
Hili lilikuwa shambulio la kushtukiza. Owo iana amani kiasi na imeepushwa na mauaji ya kiholela ambayo yanaonekana kutokea kila wiki nchini Nigeria.
Mashambulizi dhidi ya makanisa yametokea hapo awali - ilikuwa mbinu ya wanamgambo wa Kiislamu wa Boko Haram, lakini ukali wa shambulio hili umeshtua wengi.
Waabudu walikuwa wamejitokeza katika ibada yao ya Jumapili bora zaidi kwa ibada ya Pentekoste, ambayo inaashiria kuzaliwa kwa kanisa na mwisho rasmi wa msimu wa Pasaka.
"Niliona familia nzima ikiangamizwa, marafiki, jamaa, wale niliowajua," alisema Bw Nwovu.
Kwa Wakristo wa Orthodox wa Nigeria, Jumapili za kwanza za mwezi pia ni muhimu. Kawaida huwa zimejaa shukrani za kupendeza zinazoongozwa na familia na vikundi vya parokia na hii isingekuwa tofauti.
Folake Oni, 56, hakumbuki jinsi alivyonusurika kwenye shambulio hilo. Anakumbuka tu akitoka kanisani na kupelekwa hospitalini.
Binti yake Elizabeth Ademiluka aliambia BBC kwamba mamake alikuwa na kiwewe lakini alikuwa mzima.
Siku ya Jumatatu, hali ya huzuni ilitanda mjini, huku mamia ya watu waliokuwa na wasiwasi wakiwa hospitalini na wengine kadhaa kanisani.
Bado kuna umati katika hospitali mbili za mitaa ambapo watu wa kujitolea walikimbia kuchangia damu baada ya shambulio hilo.
Lakini zaidi bado inahitajika, kilisema chama cha matibabu cha Nigeria, ambacho kimewataka watu kuchangia zaidi katika hospitali za ndani.
Kila mtu anaonekana kumfahamu mtu ndani ya hospitali hiyo ambapo wengi wamejeruhiwa vibaya na wengine wanapigania maisha yao.
Wengi wa walionusurika katika Kituo Kikuu cha Matibabu cha Shirikisho (FMC) huko Owo wamepigwa risasi katika miguu yote miwili, wengine huenda wasitembee tena.
Kuna ghadhabu inayoonekana, ambayo nyingi imeenea kwenye mitandao ya kijamii, ambapo watu walifuata shambulio hilo kwa mshtuko jinsi lilivyotokea.
Baadhi ya watoto waliouawa hawakutambulika - risasi za kiwango cha juu zilitawanya nyama na mifupa, mfanyakazi wa matibabu katika FMC aliambia BBC.
"Ujasiri wa Nigeria wa kuchukua wazazi wangu. Nitaichukia nchi hii daima!!!!! Ni ahadi!," alisema mtumiaji mmoja wa Twitter.
Hasira juu ya mauaji hayo imechochewa zaidi na picha za Rais Muhammadu Buhari, Makamu wa Rais Yemi Osinbajo na wanachama wengine wa chama tawala cha All Progressives Congress (APC) wakila katika dhifa ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na rais, saa chache baada ya shambulio hilo.
Katika moja ya picha, wanasiasa hao waliovalia mavazi ya rangi wakitabasamu. Kongamano la kumchagua mgombea urais wa chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwaka ujao linaendelea mjini Abuja.
Bw Buhari ametoa taarifa ya kulaani shambulizi hilo, kitendo ambacho Wanigeria wengi wamezoea sasa, ikizingatiwa kutokea mara kwa mara kwa mauaji kama hayo.
Akiwa amechaguliwa kwa ahadi za kumaliza ukosefu wa usalama, changamoto za usalama za Nigeria zimezidi kuwa mbaya chini ya Bw Buhari, ambaye anakaribia mwisho wa uongozi wake Mei mwaka ujao.
Magenge yenye silaha ambayo yanaendesha shughuli zake kote nchini huwa hayawajibishwi na hakuna aliye na matumaini yoyote kwamba wauaji wa Owo watalipia unyama huo.
Macho yote sasa yanaelekezwa kwa gavana wa jimbo hilo, Rotimi Akeredolu, ambaye ameapa kuwasaka wauaji hao.
Yeye ni mmoja wa magavana wa kusini ambao wamekuwa wakikosoa sana shughuli za wafugaji, ambao hutoka kaskazini. Alizua tafrani kubwa mwaka jana alipowaamuru waondoke kwenye misitu ya jimbo hilo, akiwatuhumu kwa uhalifu.
Hakuna kitu kinachowahusisha wafugaji na mashambulizi ya kanisa, ambao ni rahisi kuachiliwa kwa mauaji hayo. Hata hivyo, wameshutumiwa kwa mashambulizi kama hayo siku za nyuma, hasa katikati mwa Nigeria, ambako mzozo kati ya wafugaji na wakulima umekuwa mkali sana.
Wauaji hao walikuwa wamevalia suruali ya kaki inayotumiwa na vikundi vingi vya wanamgambo wa Nigeria, alisema Bw Nwovu, hivyo wangeweza kuwa mtu yeyote.
Shambulio hilo linakuja wiki moja baada ya mkuu wa Kanisa la Methodist nchini Nigeria kutekwa nyara, pamoja na makasisi wengine wawili kusini-mashariki mwa nchi hiyo, na kuachiliwa baada ya kulipa dola 240,000.
Pia, wiki mbili zilizopita, makasisi wawili wa Kikatoliki walitekwa nyara huko Katsina, jimbo la nyumbani kwa Rais Buhari kaskazini mwa nchi hiyo na bado hawajaachiliwa.
Hili linaweza kuhisi kama wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya kanisa, na waumini kama Bw Nwovu wanatikiswa.
"Siwezi kurudi kanisani kutokana na nilichokiona, kwa sasa," alisema.
"Lakini siwezi kuacha kumwabudu Mungu," aliongeza.