logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Jamaa taabani kwa kutishia kumnyonga mkewe na kuuchoma mwili wake

Mzozo ulianza baada ya mshtakiwa kushuku kuwa mkewe alikuwa anatoka kimapenzi na mwanaume mwingine.

image
na Samuel Maina

Habari09 June 2022 - 04:37

Muhtasari


  • •David Kipng’etich Bett alishtakiwa mbele ya hakimu wa mahakama ya Kibera Jacqueline Muthoni Ojwang na kukanusha mashtaka.
  • •Kulingana na upande wa mashtaka, mzozo huo ulianza baada ya mshtakiwa kushuku kuwa mkewe alikuwa akitoka kimapenzi na mwanaume mwingine.
David Kipng’etich Bett katika mahakama ya Kibera mnamo Juni 8

Mwanamume aliyetishia kumnyonga mkewe na kuuchoma mwili wake alifikishwa mahakamani siku ya Jumatano.

David Kipng’etich Bett alishtakiwa mbele ya hakimu wa mahakama ya Kibera Jacqueline Muthoni Ojwang na kukanusha mashtaka.

Kulingana na stakabadhi za mashtaka zilizosomwa na karani wa mahakama Evans Koech mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo Mei 15 katika eneo la Amboseli,  kaunti ndogo ya Dagoretti, Kaunti ya Nairobi.

Kipng’etich anadaiwa  kutishia kumuua mkewe Peris Chepkoech .

 "Ulitishia kumnyonga Peris Chepkoech Kuyioni hadi kufa na kuuchoma mwili wake katika nyumba yako ya kupanga," Koech alisema.

Kulingana na upande wa mashtaka, mzozo huo ulianza baada ya mshtakiwa kushuku kuwa mkewe alikuwa akitoka kimapenzi na mwanaume mwingine.

Upande wa mashtaka unasema mshtakiwa aliibua suala hilo kwa mlalamikaji na wakasuluhisha kwa amani kwa ajili ya ndoa na watoto wao.

Hata hivyo, siku hiyo ya tukio, Bett anaripotiwa kumtumia mkewe ujumbe wa kutatanisha akionyesha kwamba angemuua kutokana na pesa alizomtumia kwa ajili ya karo ya shule.

Mshtakiwa alidai maelezo kutoka kwa mkewe kuhusu jinsi alivyotumia pesa.

Karatasi za mahakama zinaonyesha kuwa hapo awali Bett aliwahi kumpiga mlalamishi vibaya kichwani na kujaribu kumkata mkono wake wa kushoto.

Hakimu alimwachilia kwa bondi ya Sh200,000 au dhamana ya pesa taslimu Sh100,000 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.

Aliagiza kesi hiyo itajwe tena Juni 29 kwa maelekezo zaidi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved