Shule ya upili ya Uhuru iliyoko jijini Nairobi, ilifungwa Jumatatu kwa muda usiojulikana kufuatia kifo cha mwanafunzi mmoja katika hali tatanishi.
Polisi pia wanachunguza chanzo cha moto uliozuka katika shule hiyo na kuteketeza mabweni mawili Jumapili usiku baada ya kifo cha mwanafunzi huyo.
Polisi walisema kuwa mwanafunzi huyo hakuathiriwa na moto na bado hawajabaini chanzo cha kifo hicho.
Mashahidi na polisi walisema mwanafunzi huyo alikuwa ametoka uwanjani kushiriki mpira wa vikapu na kuwaambia marafiki zake kuwa hajisikii vizuri.
Inasemekana kuwa mwanafunzi huyo alienda kulala lakini akapoteza fahamu kabla ya kushughulikiwa katika Zahanati ya shule.
Hakukuwa na mhudumu wa afya pale shuleni, jambo ambalo liliwalazimu Wasimamizi wa shule kumpeleka katika hospitali ya karibu ambapo ilithibitishwa kuwa amefariki.
OCPD wa Buruburu Francis Ngugi Kamau alisema wanachunguza kifo hicho.
"Mwanafunzi huyo alikuwa ametoka kucheza mpira wa kikapu mwendo wa saa kumi na moja jioni na kumwambia mwanafunzi mwenzake kuwa hajisikii vizuri kabla ya tukio hilo kutokea," alisema.
Aliongeza kuwa wanapanga kufanya uchunguzi wa mwili wa marehemu ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
Kifo na tukio la moto shuleni hapo liliwalazimu taasisi hiyo kufungwa huku uchunguzi ukiendelea.
Kamau alisema moto huo ulizuka kutoka kwa bweni moja mwendo wa saa nne kasorobo usiku na kuteketeza vyumba vilivyokuwa na wanafunzi 119 wa kidato cha nne.
Wataalamu wa moto walitembelea shule hiyo kuchunguza chanzo cha moto huo.