logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wahubiri, wenye klabu wawekwa rumande kisa usumbufu wa kelele kwa umma

Baada ya umma kuteta, NEMA ilifanya operesheni na kuwatia nguvuni wahubiri wawili pamoja na vipaza sauti vyao kanisani.

image
na Davis Ojiambo

Habari30 June 2022 - 10:19

Muhtasari


  • • Baada ya umma kuteta kwa NEMA kwamba kanisa hilo lilikuwa linasumbua kwa kelele, operesheni ilifanywa na wahubiri hao kutiwa mbaroni.
  • • Watano hao wanakabiliwa na faini ya takribani elfu 33 pesa za Kenya ama kufungwa jela miaka isiyozidi 15, au yote mawili.

Mahakama moja nchini Uganda inawashikilia wahubiri wawili na wamiliki wa kumbi za burudani watatu kwa kile kilisemekana kuwa na kelele zilizopitiliza kutoka sehemu za watano hao.

Vyombo vya habari kutoka nchini humo viliwatambua wahubiri hao wanaomiliki kanisa katika mji wa Katabi na wamiliki wa klabu katika mji wa Kololo ambao waliwekwa kwenye rumande kwa muda wa wiki mbili kwa kuchafua hewa kupitia kelele za juu zinazotoka maeneo yao ya kazi.

Wakisomea mashtaka yao katika mahakama iliyoko barabara ya Buganda, hakimu mkuu alisema watano hao ni washukiwa wa kuchafua hewa kwa kelele ambapo wote kwa pamoja walikana mashtaka yao kupelekea kuwekwa rumande.

Inasemekana washukiwa hao wa uchafuzi wa hewa kupitia kelele walishtakiwa na bodi ya kitaifa inayosimamia mazingira NEMA ambapo walitiwa nguvuni wiki jana katika msako unaoendelea nchini humo dhidi ya wachafuzi wa mazingira kwa kelele za kukera.

“Walishtakiwa kwa ‘kutofanya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii, kujihusisha na shughuli zinazosababisha au kuzidisha uchafuzi wa mazingira, kumwaga na kutoa uchafuzi wa mazingira, kushindwa kutekeleza hatua za udhibiti, maagizo, matangazo na uboreshaji wa mazingira kama inavyotakiwa na Kitaifa kama inavyotakikana na Sheria ya Mazingira, 2019’” Gazeti moja la nchini humo liliripoti.

Kulingana na sheria za NEMA nchini Uganda, inahitaji taasisi kama vile maeneo ya ibada, shughuli za burudani na uzalishaji ama kuwasilisha mihutasari ya mradi au kufanya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii ili kuwezesha mamlaka husika kuongoza shughuli zao ili kuhakikisha kuwa masuala ya mazingira ikiwa ni pamoja na kelele, hewa na maji haviathiriki.

Wahubiri hao pamoja na wajasiriamali hao sasa wanakabiliwa na faini ya takribani elfu 33 pesa za Kenya ama kufungwa jela miaka isiyozidi 15, au yote mawili.

Mkuu wa mawasiliano ya umma wa NEMA nchini humo alisema kwamba wananchi ndio walilalamika kwao kwamba kanisa hiyo imeshindwa kudhibiti kelele zinazotokana na shughui zao za kumuabudu Mungu, ilibidi shirika hilo lifanye operesheni katika eneo hilo ambapo waliwatia nguvuni wahubiri hao wawili pamoja na vipaza sauti vyao.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved