Watu watatu wamethibitishwa kufariki katika ajali mbaya zilizohusisha magari manne katika eneo la Kosachei kwenye Barabara kuu ya Eldoret-Webuye.
Ajali hiyo ilihusisha lori mbili na matatu mbili.
Mkuu wa polisi wa Uasin Gishu Ayub Gitonga alisema matatu moja iligonga lori iliyokuwa ikielekea Webuye.
Dakika chache baadaye matatu nyingine iliyokuwa inatoka upande wa Webuye ikielekea Eldoret ilisimama katika eneo la tukio lakini pia ikagongwa na lori lingine lililokuwa likienda kwa kasi kuelekea Eldoret.
Lori la pili lilisukuma matatu kwenye mtaro na kuanguka juu yake na kuwafungia abiria.
Wengi wa waliojeruhiwa tayari wameondolewa katika eneo la tukio na kupelekwa hospitalini.
Gitonga alisema zaidi ya watu kumi wamejeruhiwa katika ajali hiyo.
Ajali hiyo imesababisha msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara kuu ya Eldoret-Webuye.