Bahati afurushwa kutoka kwa mkutano wa Azimio Mathare

Alilazimika kugura mkutano huo hata kabla ya kutoa hotuba.

Muhtasari

•Mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi wakuu wa Azimio ulifanyika katika eneo bunge lake la Mathare.

•Baada ya kusimama pale kwa muda katika hali ya kuchanganyikiwa Bahati alikubali kushuka chini.  

Kelvin Bahati Kioko anayelenga ubunge Mathare kupitia chama cha Jubilee
Msanii Bahati Kelvin Bahati Kioko anayelenga ubunge Mathare kupitia chama cha Jubilee
Image: Instagram screenshot

Jumatatu mwanamuziki Kelvin 'Bahati' Kioko alifukuzwa kutoka kwa mkutano wa Muungano wa Azimio- One Kenya jijini Nairobi.

Bahati ambaye anawania ubunge wa Mathare kwa tikiti ya Jubilee alilazimika kugura mkutano huo hata kabla ya kuwahutubia wafuasi wake.

Mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi wakuu wa Azimio ulifanyika katika eneo bunge lake la Mathare.

Mgombea ugavana wa Nairobi Polycarp Igathe, mgombea useneta Edwin Sifuna na mbunge wa sasa wa Mathare Tom Oluoch ni baadhi ya wanasiasa waliokuwa pale.

Wanasiasa hao walikuwa wameandaa jukwaa juu ya magari yao.

Katika video ya mtandaoni iliyofikia Radio Jambo,  viongozi kadhaa wanaonekana wakimiashiria msanii huyo aondoke jukwaani.

Bahati alikuwa akipungia mkono umati wa watu waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya mkutano huo wakati alipofukuzwa.

Watu waliokuwa wamejumuika pale ambao inaonekana hawakupendezwa na uwepo wa Bahati walisikika wakimpigia kelele.

Baadhi ya viongozi waliokuwa pale walitumia mikono yao kumwelekeza msanii huyo ashuke kutoka kwa jukwaa.

Baada ya kusimama pale kwa muda katika hali ya kuchanganyikiwa Bahati alikubali kushuka chini.  

Baadhi ya wasaidizi wake walionekana wakimzuia kutokana na umati ambao ulikuwa umezingira eneo hilo.

Haya yanajiri wiki moja baada ya Bahati na katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna kurushiana maneno makali.

Sifuna alikuwa ametangaza kuwa Azimio alikuwa ametulia na mbunge wa sasa wa Mathare Anthony Oluoch kupeperusha bendera yao katika uchaguzi wa Agosti 9.

"Zoning ilifanyika kikamilifu hata hapa Mathare tumekubaliana kuwa ni eneo la ODM. Tuna mgombea mmoja tu huko Mathare naye ni Oluoch, huyu kijana anayeitwa Bahati ni mdogo wangu na tutazungumza. Nitahakikisha kuwa mtafutie nafasi nyingine ndani ya serikali ya Azimio," Sifuna alisema.

Bahati alimjibu Sifuna akisema hatajiondoa katika kinyang'anyiro hicho hata kama alimtaka ajiepushe na masuala ya wanaowania chama cha Jubilee.

"Hoja na ujumbe wangu kwa watu wa Mathare ni kwamba bado niko kwenye kinyang'anyiro na nitashiriki kwenye kura. Sitoachia mtu yeyote".