Mgombea ugavana wa Nairobi Johnson Sakaja sasa anaweza kupumua baada ya kesi ya kupinga kufuzu kwake kielimu kutupiliwa mbali.
Jaji Anthony Mrima alisema mlalamishi Dennis Wahome alishindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa cheti cha shahada ya Sakaja ni ghushi.
Mahakama ilisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haikufanya makosa kumuidhinisha Sakaja kuwania ugavana wa Nairobi.
Mrima alisema ni jukumu la mwombaji kuthibitisha kesi zilizofikishwa mahakamani. Mahakama ilitupilia mbali ombi hilo kwa msingi wa ukosefu wa uthibitisho.
"Mahakama imegundua kuwa IEBC haikukosea kumuidhinisha Sakaja kuwania kiti cha ugavana Nairobi," aliamuru Jaji Anthony Mrima.
Kidagaa kilianza kumuozea Sakaja baada ya kuwasilishwa kwa maombi manne ya kutaka kufutwa kwa kibali chake kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutokuwa na sifa za elimu.
Kamati ya Kusuluhisha Mizozo ya IEBC inayoongozwa na Wafula Chebukati ilianza kusikiliza kesi baada ya kuunganisha maombi yote manne.
Mmoja wa waombaji, Dennis Wahome, alidai kuwa shahada ya Sakaja ambayo inasemekana aliipata kutoka Chuo Kikuu cha Team nchini Uganda ilikuwa ghushi.
Seneta huyo alisisitiza kuwa ana Shahada ya Kwanza ya Sayansi katika Usimamizi aliyokabidhiwa na Chuo Kikuu cha Team.
Hata hivyo, mahakama ya IEBC ilitupilia mbali malalamishi yaliyowasilishwa dhidi ya Sakaja kuhusu vyeti vyake vya masomo.
Wahome aliwasilisha tena ombi la kutaka IEBC isichapishe jina la Seneta Johnson Sakaja kwenye karatasi za kupigia kura.
Mnamo Julai 1, 2022, mahakama kuu ilikataa kuzuia kwa muda IEBC kujumuisha jina la Sakaja kwenye kura ya kinyang'anyiro cha ugavana Nairobi.
Badala yake, Jaji Anthony Mrima aliagiza kwamba kesi iliyowasilishwa na Wahome ifuatiliwe haraka na kusikizwa wiki jana ambayo na baadae ikasukumwa hadi Jumanne wiki hii.
Tangu wakati huo mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amekataa kubatilisha kibali cha Sakaja.