Maafisa wawili wa polisi mnamo Alhamisi waliambia mahakama ya Nairobi kuwa usiku wa kuamkia siku ya mauaji ya Sharon Otieno, msaidizi wa Gavana wa Migori Okoth Obado alitoa ripoti katika kituo cha polisi cha Uriri akidai alikuwa mwathiriwa wa kutekwa nyara.
Msaidizi huyo- Michael Oyamo-alidai kutekwa nyara na wanaume watatu baada ya kukutana na Sharon huko Rongo.
Mmoja wa maafisa hao aliambia mahakama kuwa alitilia shaka ripoti ya kutekwa nyara kwa Oyamo kwa sababu maelezo hayakuwa yakijumlishwa.
Obado, wasaidizi wake Oyamo na Caspal Obiero wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya Sharon na mtoto wake aliyekuwa tumboni.
Maelezo ya kosa hilo yanaonyesha kuwa kati ya Septemba 3-4, 2018,maeneo ya Owade huko Rachuonyo, kaunti ya Homa Bay, pamoja na wengine ambao hawakuwa mbele ya mahakama, waliwaua wawili hao.
Mwili wa Sharon ulipatikana mnamo Septemba 4 kwenye kichaka karibu na mji wa Oyugis.
Afisa Howard Omwoha Alhamisi alimweleza hakimu wa kesi Cecilia Githua kwamba mnamo Septemba 4, naibu kamanda wa polisi aliyetambuliwa kama Ojwang’ alifika katika afisi ya kuripoti akiwa na Oyamo.
Kamanda wa polisi wa utawala, ambaye sasa ni marehemu, alimtambulisha Oyamo kama msaidizi wa kibinafsi wa Obado.
Ojwang alimwambia afisa Omuoha kwamba Oyamo alikuwa na ripoti ya kuhusu kilichofanyika na inafaa kurekodiwa katika Kitabu cha Matukio.
Ni wakati huo ambapo Oyamo alianza kutoa maelezo ya kutekwa nyara kwake.
Alimwambia Omuoha kwamba usiku huo, alienda Rongo kukutana na Sharon, ambaye alidai kuwa mpenzi wake.
"Aliniambia alikuwa akikutana na mpenzi wake katika hoteli ya Treat House huko Rongo lakini Sharon alimpigia simu akiomba wabadilishe ukumbi hadi Graca hoteli," shahidi alisema.
Kulingana na afisa huyo, Oyamo alikuwa na tofauti fulani na Sharon. Madhumuni ya mkutano huo ilikuwa ni kutatua masuala yao.
Oyamo aliendelea kumwambia afisa huyo kwamba mtoto aliyekuwa tumboni mwa Sharon alikuwa wake, na Sharon alitaka Sh600,000 za Nyumba.Pia alitaka Sh240,000 nyingine kwa ajili ya kujikidhi kimaisha.
Matokeo ya DNA yamethibitisha kuwa mtoto wa kiume ambaye hajazaliwa alikuwa wa Obado.
“Teksi ilikuja lakini kabla hawajaondoka, Oyamo alisema alimpa Sharon Sh100,000 ili kulipia vinywaji. Baadaye walipanda teksi iliyokuwa imeegeshwa ndani la hoteli,” shahidi huyo alisema.
Kulingana na ripoti ya Oyamo, kulikuwa na wanaume watatu kwenye teksi lakini bado alipanda gari hilo akiwa na Sharon na mwanamume mwingine.
Hakutaja watu waliokuwa kwenye teksi hiyo ni akina nani lakini dereva wa teksi anadaiwa aliendesha takriban mita 200, akaondoka upande wa kushoto wa barabara na kumwamuru Oyamo atoke nje.
Wakati wote huo, kulikuwa na Toyota Axio iliyokuwa ikiwafuata. Oyamo aliamriwa kupanda huku Sharon akiachwa kwenye gari lingine.
“Oyamo aliniambia wanaume katika Axio walikuwa wakimtesa. Walimpiga na kudai Sh1.5 milioni. Walikuwa na visu lakini hawakuvitumia,” shahidi alisema alipokuwa akisimulia ripoti ya Oyamo.
Oyamo alipoteza fahamu na akajikuta katika mitaa ya Kisii asubuhi iliyofuata."
Oyamo alimweleza afisa huyo kwamba wananchi walimpeleka katika hospitali moja mjini Kisii.
Lakini daktari ambaye ametoa ushahidi katika kesi hiyo alikiri kughushi rekodi za matibabu kwa Oyamo kudanganya kwamba alishambuliwa na watu wasiojulikana usiku ambao Sharon aliuawa.
Afisa mwingine aliyetoa ushahidi katika kesi hiyo Alhamisi alimweleza hakimu kwamba ripoti ya utekaji nyara ya Oyamo haikuwa ya ukweli.
Alisema alitilia shaka ripoti yake kwa sababu ilikuwa na habari tofauti tofauti.