Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya afisa Msimamizi wa Uchaguzi wa IEBC, Daniel Musyoka.
Musyoka alitoweka mnamo Agosti 11 saa 9:45 asubuhi na mwili wake ukapatikana siku nne baadaye Mariko huko Loitoktok, Kaunti ya Kajiado.
Katika barua iliyoandikwa Alhamisi, Agosti 18, Haji pia alimwamuru Mutyambai kuwasilisha matokeo yake ndani ya siku saba.
“Kwa hiyo, mnaagizwa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo, kwa mujibu wa Ibara ya 157 (4) ya Katiba ya mwaka 2010 na kuwasilisha jalada la uchunguzi wa matokeo ndani ya siku saba tangu tarehe ya mwisho,” ilisema barua hiyo.
Haya yanajiri siku moja baada ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati kutaka uchunguzi ufanyike haraka kuhusu mauaji na kufunguliwa mashtaka kwa waliohusika.
Alisikitika kuwa ingawa Musyoka alitoweka mnamo Agosti 11 na mwili wake kupatikana mnamo Agosti 15, uchunguzi bado haujafanywa.
"Tume inapoifariji familia ya Musyoka, tunatoa wito kwa vyombo vya usalama kuchunguza haraka na kuwakamata wauaji wake," alisema.
Siku ya Jumatano, wataalamu watano wanaofanya kazi ya uchunguzi wa maiti hawakuweza kubaini kilichomuua Musyoka.