Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Roots, Justina Wamae ameendelea kufunguka kuhusu uhusiano wake na kiongozi wa chama George Wajackoyah.
Wamae sasa anadai alizungumza mara ya mwisho na bosi wake kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
"Mara ya mwisho nilifanya mazungumzo na kiongozi wa chama changu ilikuwa Agosti 3, hiyo ilikuwa kabla ya uchaguzi," alisema wakati wa mahojiano na televisheni moja siku ya Jumanne.
Wamae alidai baada ya hapo, Wajackoyah alimblock na hawajawasiliana naye isipokuwa wakati walipokutana Bomas of Kenya wakati wa kujumlisha kura - na walisalimiana tu.
"Hatujazungumza naye kuhusu masuala ya uchaguzi na chama chetu ana kwa ana," Wamae alifichua.
Uhusiano kati ya wanasiasa hao wawili umegonga mwamba na kusababisha wito wa kinidhamu kwa Wamae.
Mgogoro unahusu matamshi ya Wamae hadharani ambayo hayawiani na msimamo wa chama chao.
Miongoni mwao ni matamshi kuwa Wajackoyah aliidhinisha mgombea urais wa Azimio Raila Odinga kabla ya uchaguzi, nafasi ambayo kiongozi wa chama chake alipuuzilia mbali kama uongo.
Katika barua ya mkurugenzi wa masuala ya sheria Washika Wachira, chama hicho kilimkashifu Wamae kwa kukiuka miundo ya chama na kuchafua sifa ya chama.
Wamae, hata hivyo, alipuuzilia mbali wito huo akisema hawezi kujibu mambo madogo.
Wakati wa mahojiano Jumanne, Wamae alidai chama chake hakina mpangilio na uhamasishaji wao wa maajenti kwa uchaguzi ulikuwa duni.
"Sababu iliyonifanya kusema kuwa chama chetu hakijajiandaa ni ukweli kwamba yeye (Wajackoyah) hakutaka kuzungumza nami kama mshirika wake wa karibu,"
Wamae, hata hivyo, alisema kuwa licha ya changamoto hizo, hakuona ni busara kuzitangaza hadharani.
Anataka masuala yatatuliwe kwa kikao cha moja kwa moja na sio kwenye mitandao ya kijamii.