logo

NOW ON AIR

Listen in Live

(+video) Kirinyaga: Kijiji wafu wanazikwa kwa gunia ya Ksh 50, ukosefu wa hela za jeneza

Kirinyaga: Kijiji kimoja kiliamua kukumbatia kuzika wapendwa wao kwa gunia ya shilingi 50 kwa kukosa pesa za kununua jeneza.

image
na Davis Ojiambo

Habari31 August 2022 - 11:01

Muhtasari


  • • “Sio mtu wa kwanza kuzika kwa gunia. Anakufa asubuhi tunazika saa nane mchana. Tunanunua gunia kwa Ksh50 pekee na kumzika mtu huyo na hutuchukua dakika 20 pekee,”

Ni taarifa za kuvunja moyo sana kutoka kaunti ya Kirinyaga ambapo inaarifiwa kwamba familia moja iliamua kumzika mpendwa wao kwa kutumia gunia baada ya kukosa pesa za kununua jeneza.

Familia hiyo si ya kwanza kufanya kufuru hiyo kwani inaarifiwa kwamba katika Kijiji hicho kutokana na uhaba wa fedha, imekuwa ni kawaida kwao kumzika mtu kwa kutumia gunia ya shilingi 50 pesa za Kenya.

Kulingana na Alexander Nzomo ambaye ni mzee mmoja wa wakaazi wa Kijiji cha Ndindiruku kaunti ya Kirinyaga ambapo itikadi za kuzika kwa gunia zimekuwa zikifanyika, anasema waliamua kukumbatia matumizi ya gunia baada ya kukosa fedha za kumudu kununua jeneza.

Akizungumza katika video moja ambayo imepakiwa mtandao wa YouTube wakati wa msiba wa mkaazi mmoja Njeru Ndiga aliyeshambuliwa na mamba, Nzomo alisema uhaba wa pesa uliwasukuma kutumia gunia ila kwa bahati nzuri diwani wa eneo hilo akaingilia kati na kutoa pesa ya jeneza.

“Tulifikiria kuzika Njeru kwa gunia kwa sababu tuliangalia tukaona hakuna usaidizi huku kwao. Hakukuwa na kitu chochote ambacho tungeuza ndio tusaidie Njeru. Hapo ndio tulishauriana na kuita diwani ili atusaidie,” Nzomo alisema.

Aidha aliweka bayana kwamba huyo hakuwa mtu wa kwanza kupangiwa kuzikwa kwa gunia kwani jambo hilo limekuwa likitendeka awali.

“Sio mtu wa kwanza kuzika kwa gunia. Anakufa asubuhi tunazika saa nane mchana. Tunanunua gunia kwa Ksh50 pekee na kumzika mtu huyo na hutuchukua dakika 20 pekee,” mwingine alisema.

Wakaazi hao wakizungumza kweney video hiyo baada ya mazishi kukamilika ambapo MCA mteule wa Tebere Peter Karinga alijitolea kununua jeneza, wakaazi hao walisema marehemu alikuwa amepangiwa kupewa maziko kwa gunia kwa sababu hakuwa na kitu chochote na hakuwa amejiunga katika kikundi chochote cha kuchangisha pesa.

Viongozi wa kanisa waliwataka watu kuwajibika wakati wako hai na kufanya mipango ya kujiunga na vyama vya kuchangishiana pesa mtu anapopatwa na msiba kwani hii ndio njia pekee ya kuhakikisha yeye pia akipata msiba anapata msaada.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved