Mwanamke mmoja alidaiwa kuuawa na mumewe katika eneo la New Valley, Kitengela baada ya ugomvi wa kinyumbani.
Kulingana na majirani wa wanandoa hao, mwanamke huyo alikuwa ameenda kuosha nywele zake katika saluni moja eneo hilo na kuchukua muda mrefu kurejea nyumbani.
"Mwanamke huyo aliondoka nyumbani kwenda saluni saa moja asubuhi na akarudi saa tisa alasiri na kumkuta mume tayari yuko nyumbani," alisema Ann Njeri, mmoja wa majirani.
Njeri alisimulia kuwa wawili hao walianza kugombana baada ya mwanaume mwenye nyumba kuuliza ni kwa nini bibi huyo alikaa saluni kwa muda lakini alimwacha mtoto mchanga ndani ya nyumba hiyo.
Mwanamume huyo ambaye alikuwa amejawa na ghadhabu aliaanza kumpiga mwathiriwa huku akitishia kumdunga kisu hadi kumuua.
Mwanamke huyo alipiga uyowe akiwatahadharisha majirani. Alijaribu kutoroka lakini mumewe akamkimbiza na wakati akijaribu kumshika, mwanamke huyo alijikwaa na kuangukia jiwe.
Ingawa majirani walijaribu kumwokoa, mwanamke huyo alifariki papo hapo na kupelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali Ndogo ya Kitengela na polisi.
OCPD wa Isinya Ancient Kaloki alithibitisha kisa hicho na kuongeza kuwa mshukiwa amekamatwa na polisi na anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kitengela akisubiri kuwasilishwa kortini.
Majirani hao walifichua kwamba wachumba hao ambao wamekuwa pamoja kwa miaka miwili wamekuwa na uhusiano wa ndani na nje ulioathiriwa na unyanyasaji wa nyumbani.
Mwanamke huyo, ambaye majirani wanaamini kuwa ana umri wa chini ya miaka 20, ameacha mtoto mchanga.
Evans Wakhungu, mmoja wa wakazi katika eneo hilo, anasema kuwa amekuwa akiwaona wawili hao wakiwa pamoja na kushangaa ni kwa nini mwanamume huyo alikuwa ameoa mtoto mdogo.
Wakhungu aliwataka wanandoa kila mara kutatua masuala yao kwa amani, badala ya kuuana.
"Inasikitisha kwamba mwanamke huyo alifariki akiwa na umri mdogo. Ninawahimiza wanandoa kila mara kutafuta njia mbadala za kutatua mizozo. Kuuana sio suluhu," akasema Wakhungu.