Mgombea urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga amesema kuwa anauheshimu uamuzi wa makahama kuidhinisha ushindi wa Ruto.
Waziri huo mkuu wa zamani hata hivyo ameweka wazi kuwa hakubaliani kabisa na uamuzi ambao ulitolewa adhuhuri ya Jumatatu.
"Siku zote tumesimamia utawala wa sheria na katiba. Kuhusiana na hili, tunaheshimu maoni ya mahakama ingawa hatukubaliani vikali na uamuzi wao leo," Raila alisema katika taarifa aliyotoa Jumatatu.
Kinara huyo wa ODM alishikilia kuwa ushahidi ambao mawakili wake waliwasilisha ulikuwa wa kutopingika.
"Tunaona ni jambo la ajabu kwamba majaji waliamua dhidi yetu katika hoja zote tisa na tukio lilisababisha lugha ya kuzidisha kupita kiasi kukanusha madai yetu," aliongeza.
Raila alidokeza kuwa ataendelea kupigania demokrasia ya Kenya licha ya mahamaka kutupilia mbali kesi yake.
Pia aliwashukuru wafuasi wake kwa kusimama naye na kuwaambia atazungumza kuhusu hatua yake nyingine baadae.
"Hivi karibuni tutazungumza kuhusu mipango yetu ya kuendelea kupigania uwazi, uwajibikaji na demokrasia," alisema.
Jumatatu alasiri mahakama ya upeo iliamua kwamba uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ulikuwa halali na ulifuata sheria.
Raila alikuwa amepinga matokeo ya urais yaliyotangazwa Agosti 15 na kudai kuwa uchaguzi haukuwa wa haki.