Mvulana wa miaka 13 ajitoa uhai baada ya mamake kumzomea kwa kufeli mitihani

"Nilimuuliza kwa nini aliacha kutia bidii shuleni baada ya kupitia kadi yake ya matokeo," mamake marehemu alisema.

Muhtasari

•Kulingana na mamake marehemu, Dorcas Asmit na dadake, mvulana huyo alikasirika wakati mamake alipomhoji kuhusu kushuka kwa alama zake shuleni baada ya kufunga shule.

•Familia hiyo ilipiga nduru zilizowavutia majirani waliokimbilia eneo la tukio.

Image: HISANI

Mvulana mwenye umri wa miaka 13 alifariki kwa kujitoa uhai katika kijiji cha Kanamkemer, eneo la Lodwar wikendi.

Kulingana na mamake marehemu, Dorcas Asmit na dadake, mvulana huyo alikasirika wakati mamake alipomhoji kuhusu kushuka kwa alama zake shuleni baada ya kufunga shule.

Marehemu, Allan Kipkoech alikuwa mwanafunzi katika shule ya Harmony academy huko Lodwar.

"Nilimuuliza kwa nini aliacha kutia bidii shuleni baada ya kupitia kadi yake ya matokeo," alisema Asimit.

Alisema alienda kwa nyanyake mvulana huyo na takriban nusu saa baadaye akapokea habari kwamba mwanawe amejitoa uhai baada ya kujifungia ndani ya nyumba.

Hii ni baada ya Sharon Achemee, mzaliwa wa tatu katika familia hiyo kutaka kuingia kwenye nyumba hiyo na kugundua kuwa ilikuwa imefungwa kutoka ndani.

"Nilipogundua kuwa nyumba ilikuwa imefungwa kutoka ndani niligundua kuwa kila kitu hakikuwa sawa. Kupitia dirishani nilimwona kaka yangu akining'inia kutoka kwenye paa," Achemee alisema, na kuongeza, alikuwa amejinyonga kwa leso.

Familia hiyo ilipiga nduru zilizowavutia majirani waliokimbilia eneo la tukio.

Mwalimu Mkuu wa Harmony Academy Clinton Gichaba alisema mwanafunzi huyo, ambaye alijiunga na shule hiyo Mei mwaka huu, aliondoka shuleni akiwa katika hali ya furaha.

"Inasikitisha tumempoteza mvulana mwenye nidhamu ya hali ya juu katika umri mdogo. Tunaomba uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini chanzo halisi cha kifo," alisema.