Wakenya washauriwa kuzuru Dubai wakati wa msimu wenye shughuli ndogo za utalii

Wakenya ni miongoni mwa watalii watatu wakubwa wa Dubai.

Muhtasari

•Meneja wa utalii wa Dubai amesema msimu huo huwa wa bei nafuu zaidi kwani shughuli nyingi zinazovutia watu huwa ni bila malipo.

•Stella aliwasifu Wakenya kwa kuzingatia Dubai kama mahali pazuri pa likizo.

wakati wa hotuba yake katika hoteli ya Movenpick mnamo Septemba 22, 2022
Stella Fubara, mkurugenzi wa Operesheni za Kimataifa Afrika , wakati wa hotuba yake katika hoteli ya Movenpick mnamo Septemba 22, 2022
Image: WILFRED NYANGARESI

Ikiwa ungependa kutembelea Dubai, unashauriwa kufanya hivyo wakati wa msimu usio wa shughuli nyingi za utalii.

Meneja wa utalii wa Dubai wa kanda Stella Obinwa amesema msimu huo huwa wa bei nafuu zaidi kwani shughuli nyingi zinazovutia watu huwa ni bila malipo.

"Unapata kuenda hadi kwenye bustani nzuri na pia kupata usafiri wa bure na pia maduka makubwa huko Dubai ambayo ni chanzo cha burudani," alisema.

Pia aliongeza kuwa hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu usalama kwani Dubai imeorodheshwa miongoni mwa nchi tatu bora kwa usalama duniani.

"Usijali ukiwa likizoni Dubai. Usalama wako umehakikishwa na huwa haupatwi na woga, kila mtu anakaribishwa," alisema.

Alisema Wakenya ni miongoni mwa watalii watatu wakubwa wa Dubai.

Stella ambaye alikuwa akizungumza wakati wa maonyesho ya utalii ya Dubai jijini Nairobi aliwasifu Wakenya kwa kuzingatia Dubai kama mahali pazuri pa likizo.

Hata hivyo alibainisha kuwa hawashindani na utalii wa ndani wa Kenya.

Kuhusu uwezo wa kumudu kuzuru Dubai, alisema kwa dola 60(Sh7,200) mtu anaweza kupata hoteli ya kifahari.