Fahamu kwa nini familia ya muuguzi wa Kenya aliyekufa maji nchini Canada haitalipwa

Mwili wa Hellen Wendy uliwasili nchini Jumamosi kwa ajili ya mazishi.

Muhtasari

•Babake Wendy alisema mwili umehifadhiwa katika mochari ya Lee Funeral Home kabla ya kusafirishwa hadi Kisii ambako atazikwa.

•Bi Nyabuto alilalamika kuhusu sheria za hoteli hiyo akisema wageni wapya wanapaswa kusimamiwa wanapoogelea.

Image: FACEBOOK// HELLEN WENDY

Mwili wa muuguzi wa Kenya aliyekufa maji katika dimbwi la kuogelea nchini Canada hatimaye uliwasili nchini kwa ajili ya mazishi.

Hellen Wendy alifariki mnamo Agosti 18 alipokuwa akiogelea baada ya kutoka kazini. Wakati huo alikuwa akijirekodi kupitia kipindi cha moja kwa moja kwenye Facebook na kuwasiliana na marafiki wake walio Kenya.

Mwili wake uliwasili Jumamosi ndani ya ndege la  Ethiopian Airlines  saa 1.05 jioni (EAT) kabla ya mazishi yake huko Kisii, yaliyopangwa kufanyika Oktoba 3. Wazazi wa marehemu na wanafamilia wengine waliokuwa wamesafiri kwenda Kanada wiki iliyopita waliandamana na mwili huo ulipokuwa ukiletwa nchini.

Akihutubia waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa JKIA, babake Wendy ,John Nyabuto, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika mochari ya Lee Funeral Home kabla ya kusafirishwa hadi Kisii ambako atazikwa.

"Mchakato ulikuwa mrefu. Kufanya kila kitu na kujaza stakabadhi zinazohitajika ilikuwa inachukua muda mrefu," alisema Bw Nyabuto.

Mamake Wendy alisema walipokewa vizuri nchini Canada na kwa usaidizi wa watu mbalimbali wakafanikiwa kukamilisha hatua zilizohitajika ili hatimaye kuweza kusafirisha mwili wa binti wao hadi nyumbani.

Alisema walitembelea kidimbwi cha kuogelea ambapo binti yao  alizama na kufahamishwa kwamba hakutakuwa na fidia.

"Tulifika kwa ile swimming pool na tukaona imeandikwa 'bila kusimamiwa'. Sasa ukiingia hapo uzame ni juu yako mwenyewe, hakuna kulipwa," alisema.

Bi Nyabuto alilalamika kuhusu sheria za hoteli hiyo akisema wageni wapya wanapaswa kusimamiwa wanapoogelea.

"Kama ni mgeni ameenda pale, ni aje mwenye dimbwi anaweza akaacha hivo tu bila kusimamiwa?" alihoji.

Aliongeza, "Tuliongea naye akasema tuangalie alivyoandika hapo."

Mwili wa Wendy umeratibiwa kuzikwa nyumbani kwao Kisii wiki  ijayo. Babake marehemu alisema familia itashiriki kikao na kukubaliana kuhusu tarehe rasmi ya mazishi.