Mbunge wa Olkalau David Kiaraho anadai alitekwa nyara akiwa kwenye gari lake huku akiwa ameshikiwa bunduki na kuibiwa Sh700,000 pamoja na vitu vingine vya thamani jijini Nairobi.
Aliripoti kisa hicho Jumapili asubuhi katika kituo cha polisi cha Karen ambapo alisema alitekwa nyara usiku na kuzungushwa kwenye gari lake kabla ya kuporwa pesa taslimu, kadi ya ATM na vitu vingine vya thamani na baadaye kutelekezwa bila majeraha yoyote.
Mbunge huyo aliambia polisi kuwa alikuwa ameondoka kwenye kilabu maarufu kando ya barabara ya James Gichuru na kufika kwenye makutano ya Waiyaki Way mwendo wa saa nane asubuhi alipopunguza mwendo.
Alikuwa peke yake ndani ya gari kisha akazuiwa na jambazi mwenye silaha akiwa amemnyooshea bunduki.
Mshambuliaji huyo alimuamuru ashushe dirisha lake na akakubali na baadaye akaagizwa afungue milango.
Baadae majambazi wengine wawili waliingia kwa nguvu ndani ya gari lake la magurudumu manne na kumwamuru aendeshe Waiyaki Way hadi eneo la Muthiga huko Kikuyu.
Alisema genge hilo baadaye lilidhibiti gari hilo na kumfumba macho wakidai pesa, bunduki na vitu vingine vya thamani kutoka kwake walipokuwa wakizunguka kwa karibu saa mbili.
Majambazi hao walivamia gari lake na kupata Sh700,000 zilizokuwa zimefichwa chini ya kiti cha dereva na kuwafanya kubadilisha hisia zao na kuonyesha urafiki.
Alizungumza nao akiwasihi wasimdhuru na baadaye wakaendesha gari lake hadi Barabara ya Miotoni huko Karen ambapo walimtelekeza humo.
Genge hilo lilikuwa limefanya mipango ya kupata gari la kugura ambalo lilikuwa likiwangojea mahali hapo.
Waliruka kwenye gari jeupe la saluni na kuondoka zao wakimuacha Kiaraho kwenye kiti cha nyuma akiwa amefumba macho.
Aliokolewa na walinzi walioshuhudia tukio hilo na baadaye akaendesha gari hadi kituo cha polisi ambako alitoa taarifa hiyo.
Hatukuweza kumpata Jumanne na Jumatano kwa maoni yake kuhusu masaibu hayo kwa kuwa simu yake ya mkononi haikuwa inaingia.
Polisi wanaoshughulikia kesi hiyo walisema alikuwa amewaambia hana nia ya kuzifuatilia zaidi pesa hizo kwa sababu washambuliaji walikuwa wamemuokoa.
Aliwaambia polisi pesa walizomwibia "zitafutwa na kupatikana" maadamu yu hai na hataki kuzifuatilia zaidi.
"Hajarudi kwa taarifa zaidi kama ilivyokubaliwa na alionyesha yuko sawa na hataki ifuatiliwe kwa sasa," afisa anayefahamu uchunguzi huo alisema.
Polisi wanaamini genge lililohusika na tukio la hivi punde ndilo lile lile ambalo limekuwa likilenga magari ya hali ya juu jijini.