Huzuni huku waombolezaji wakitazama mwili wa Hellen Wendy kabla ya mazishi kufanyika leo

Baadhi ya waombolezaji waliangua kilio kikubwa pindi baada ya kutazama mwili wa Wendy.

Muhtasari

•Mwili wake ulikuwa umehifadhiwa katika mochari ya Canada hadi wiki jana wakati familia yake ilipoenda kuuchukua kwa ajili ya mazishi. 

•Hafla ya mazishi ya Wendy itafanyika leo Jumanne, takriban mwezi moja unusu baada yake kuaga dunia huko Canada.

Image: FACEBOOK// HELLEN WENDY

Mwili wa muuguzi wa Kenya aliyekufa maji wakati akiogelea kwenye bwawa nchini Canada hatimaye ulifikishwa nyumbani kwao Motonto, kaunti ya Kisii kabla ya mazishi yaliyoratibiwa kufanyika leo, Jumatano.

Hellen Wendy Nyabuto alikuwa akishirikisha marafiki wake katika kipindi cha moja kwa moja kwenye  Facebook mnamo Agosti 18 wakati alipokumbana na kifo chake baada ya kuwezwa na nguvu za maji na kwa bahati mbaya kuzama.

Mwili wake ulikuwa umehifadhiwa katika mochari ya Canada hadi wiki jana wakati familia yake ilipoenda kuuchukua kwa ajili ya mazishi. 

Baada ya kufanikiwa kuuchukua mwili, wazazi wa marehemu waliusafirisha kwa ndege la Ethiopian Airliness na kuwasili JKIA  Jumamosi.

Mwili wa Wendy ulilazwa katika chumba cha Lee hadi Jumanne wakati ulipochukuliwa na kusafirishwa hadi nyumbani kwao Kisii.

Wanafamilia, majirani, marafiki na wanakijiji waliokuwa wamekusanyika nyumbani kwa wazazi wa marehemu siku ya Jumanne walizidiwa na hisia walipokuwa wakipanga foleni kuutazama mwili wa mwanadada huyo mdogo.

Baadhi ya waombolezaji  walionekana wakiangua kilio kikubwa pindi baada ya kutaza mwili wa marehemu uliokuwa umewekwa nje.

Hafla ya mazishi ya Wendy itafanyika leo Jumanne, takriban mwezi moja unusu baada yake kuaga dunia huko Canada.

Wazazi wa marehemu  waliandamana na mwili wake ulipokuwa ukiletwa nchini siku ya Jumamosi, wiki jana.

Akihutubia waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa JKIA, babake Wendy ,John Nyabuto, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika mochari ya Lee Funeral Home kabla ya kusafirishwa hadi Kisii ambako atazikwa.

"Mchakato ulikuwa mrefu. Kufanya kila kitu na kujaza stakabadhi zinazohitajika ilikuwa inachukua muda mrefu," alisema Bw Nyabuto.

Mamake Wendy alisema walipokewa vizuri nchini Canada na kwa usaidizi wa watu mbalimbali wakafanikiwa kukamilisha hatua zilizohitajika ili hatimaye kuweza kusafirisha mwili wa binti wao hadi nyumbani.

Alisema walitembelea kidimbwi cha kuogelea ambapo binti yao  alizama na kufahamishwa kwamba hakutakuwa na fidia.

"Tulifika kwa ile swimming pool na tukaona imeandikwa 'bila kusimamiwa'. Sasa ukiingia hapo uzame ni juu yako mwenyewe, hakuna kulipwa," alisema.

Bi Nyabuto alilalamika kuhusu sheria za hoteli hiyo akisema wageni wapya wanapaswa kusimamiwa wanapoogelea.

"Kama ni mgeni ameenda pale, ni aje mwenye dimbwi anaweza akaacha hivo tu bila kusimamiwa?" alihoji.

Aliongeza, "Tuliongea naye akasema tuangalie alivyoandika hapo."